Zitto Kabwe Apasua Jipu Kutekwa Kwa Msaidizi Wake.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe ameitaka Serikali ya Tanzania kuangalia kwa uzito suala la kutekwa kwa raia wa Kenya anayeishi Tanzania, Raphael Ongagi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Julai 1, 2019 jijini Dar es Salaam, Zitto amesema masuala ya utekaji yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa nchi ya Tanzania.

Amesema Tanzania haipaswi kuwa na taswira hiyo kwa mataifa mengine hasa nchi jirani ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo katika mambo mengi.

Kutokana na hali hiyo, Zitto amewataka watekaji hao kumwachia huru kwani hana taarifa zake wanazozihitaji.

Raia huyo wa Kenya anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam, wakati akitoka shuleni kwa watoto wake kwenye kikao cha wazazi.

“Siku mbili baada ya Raphael kutekwa, akaunti zangu za mitandao ya kijamii zilidukuliwa na Raphael alikuwa na password zangu, hata hivyo hana taarifa zozote juu yangu hivyo ninawaambia watekaji hawawezi kupata taarifa zozote juu yangu kutoka kwa Raphael kwasababu watamtesa bure na hana taatifa ambazo anaweza kuwapa.

‪“Naamini wananisikia, hivyo wamuachie na kama kuna taarifa zozote wanazoona zina makosa waniite mwenyewe kwa taratibu za serikali mimi nitawapa hizo taarifa,” amesema Zitto

Amesema kuna watu wamefikia kusema rasilimali fedha zake zote zinapita kwa Raphael ambapo amesema hahusiki na chochote ni vyema wakamuita mwenyewe kama hilo ndiyo dhumuni lao.

Akielezea namna alivyokutana na Raphael, Zitto amesema ni raia wa Kenya ambaye tangu mwaka 2002 alikuja nchini na alipata marafiki wengi wa Tanzania na hata kufunga ndoa na Mtanzania.

“‪Baada ya kuamua kuingia kwenye biashara aliendelea kuwa mtu wangu wa karibu na mpaka anatekwa tumekuwa bado ni watu wa karibu hakuwa anajihusisha na siasa kwa namna yoyote,” amesema Zitto.

Hata hivyo, Zitto amesema anawasihi watekaji hao wamuache Raphael mahali kisha wao watakwenda kumchukua.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post