ZAIDI YA DOLA TRILIONI 1.4 HUPOTEA KILA MWAKA KWA NJIA YA RUSHWA BARANI AFRIKA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi  ya dola trilioni  1.4  zinapotea  kila mwaka kwa  njia ya rushwa barani  Afrika.

Hayo yalisemwa  Julai 11,2019 jijini Dodoma   na Naibu  Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano  wa  Afrika Mashariki  Dokta Damas  Ndumbaro katika ufunguzi wa  siku Maalum ya Mapambano dhidi ya rushwa kwa nchi za Umoja wa  Afrika.

Dokta Ndumbaro amesema tathmini iliyotolewa na Umoja wa  Afrika mwaka 2014 inaonesha kwamba zaidi  ya Asilimia 25% ya  GDP ya nchi za Afrika inapotea kila mwaka  na jumla ya Dola bilioni 148 zinapotea kila mwaka  kwa njia ya rushwa.

Aidha ,Dokta Ndumbaro amesema   kutokana na  ripoti inayohusu upotevu wa fedha na rasilimali iliyotoka Februari,2019[Illicit Finacial Flow Report for Africa]inaonesha kuwa Afrika inakadiriwa kupoteza kiasi cha Dola Bilioni  1.2 hadi kufikia Dola Trilioni 1.4 kwa Mwaka.

Hata hivyo Dokta Ndumbaro amesema Tanzania inaonekana kuongeza kiwango cha utawala bora kwa kupata  alama hamsini na nane na nusu kwa mia moja   [58.5/100   ]na kuwa nchi ya 14 kati ya nchi 54 kwa mwaka 2018  ikilinganisha na mwaka 2017  ambapo Tanzania ilipata alama hamsini na saba na nusu kwa mia moja[ 57.5/100]  na  kuwa nchi ya 17 katika bara la Afrika kwa mujibu wa ripoti ya  MO Ibrahim Index Of African  Governance[IIAG].

Dokta Ndumbaro ameendelea kusema kwa mujibu wa  ripoti  zinazotolewa na Transparency International [CPI]ilionesha kuwa ndani ya miaka  mitatu[3]tangu 2015  hadi 2018 Tanzania imepanda hatua  18ambapo mwaka 2015 ilishika nafasi  ya 117 kwa kupata asilimia  30% wakati mwaka  2018  imeshika  nafasi ya 99 kati  ya  nchi 180  duniani  kwa kupata alama 36   huku upande  wa nchi za Afrika Mashariki ikishika nafasi ya pili ikitanguliwa na Rwnda.

Utafiti mwingine wa Taasisi ya ndani ya nchi REPOA [AFROBAROMETER],2017 inaonesha wananchi 7 kati  ya  10  [71%] Ya   waliohojiwa  walisema  ushiriki wa serikali katika mapambano dhidi ya rushwa  ni nzuri  ambapo imeongezeka kwa asilimia 37 ya kwenye matokeo yaliyotolewa mwaka 2014.

Katika  hatua nyingine,matokeo ya utafiti  uliofanywa na TWAWEZA Mwaka 2017 umebainisha asilimia 85%  ya wananchi waliohojiwa walieleza kuwa rushwa imepungua  ikilinganisha na asilimia 11%  ya waliohojiwa  mwaka 2014.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU hapa nchini Diwani Athuman amesema  Tsh.Bilioni 86 ya Mishahara hewa zimeokolewa huku akiwataka wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Aidha ,Bw.Athuman amebainisha changamoto zinazoikabili TAKUKURU  ikiwa ni pamoja na mashahidi kutotoa Ushahidi Mahakamani,na  ufinyu wa bajeti.

Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali Prof.Juma Musa Assad amesema rushwa ni adui wa haki hivyo ni wajibu  wa kila mmoja kujidhatiti katika mapambano dhidi ya rushwa huku pia akiiomba serikali kuongeza bajeti katika mapambano hayo.

Akifunga   siku Maalum ya Mapambano dhidi ya rushwa  kwa nchi za Umoja wa  Afrika , Naibu Waziri wa ofisi ya Rais,Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala Bora Dokta Mary Mwanjelwa ametoa   wito kwa watanzania kuwa askari katika mapambano dhidi ya rushwa huku pia akitoa rai kwa bodi ya Umoja wa Afrika ya Mashariki kwa udhihirisho kuwa siku ya mapambano dhidi ya Rushwa ni muhimu hivyo ni wajibu kila mmoja kushiriki kikamilifu.

Siku Maalum ya Mapambano dhidi ya rushwa  kwa nchi za Umoja wa  Afrika  imeenda sambamba na kauli mbiu isemayo”Kuelekea kwenye Msimamo wa Pamoja wa Afrika  kuhusu urejeshwaji wa Mali”ambapo kwa hapa Tanzania maadhimisho hayo yakifanyika ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni jijini Dodoma  huku wadau mbalimbali wakihusishwa ushiriki hasa vijana kwani asilimia 63% ya Watanzania ni Vijana.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527