WAZIRI MPINA AWATANGAZIA VITA WAVUVI HARAMU


Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Luhanga Mpina ametangaza vita dhidi ya wavuvi haramu huku akisema hata  akitokea akauawa atateuliwa waziri mwingine atakayeendelea mapambano hayo.

Kauli hiyo ya Waziri Mpina ameitoa kufuatia tukio la mauaji ya watu wanne katika mapambano kati ya wakazi wa Kisiwa cha Siza wilayani Ukerewe na maofisa wa kikosi cha kupambana na uvuvi haramu wa kanda hiyo.

Waliofariki ni pamoja na ofisa mfawidhi wa rasilimali za uvuvi kanda ya Ukerewe, Ibrahim Nyangali (38). Wengine ni Damian Joseph (18), Malanja Malima (18) na Chrisant Christian (47).

Tafrani hiyo ilitokea baada ya maofisa hao waliofika wakitokea Kisiwa cha Ghana kwa ajili ya operesheni hiyo ya kusaka nyavu zinazotumika katika uvuvi haramu.

Jana Jumatano, Julai 24, 2019, Waziri Mpina aliwaongoza waombolezaji kuaga mwili wa ofisa huyo visiwani Ukerewe mkoani Mwanza ambapo alitumia fursa hiyo kutangaza mapambano dhidi ya wavuvi haramu.

“Nawapa pole sana wote katika hili tukio lililotokea. Hamuwezi kushindana na Serikali na hapa natangaza kwamba suala la uvuvi haramu ndio linaanza leo (jana),” alisema Waziri Mpina

“Damu ya hawa, damu ya maofisa iliyomwagika na wananchi watatu iliyomwagwa itaendelea kuwalilia wavuvi haramu wa Tanzania.”

Akizungumza kwa msisitizo, Waziri Mpina alisema, “Na leo (jana) natangaza vita haramu, vita mpya  na tutawasaka kila mahali, tutaimarisha sekta zote kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa na hata mkiniua leo atateuliwa waziri mwingine, hamuwezi kupona kwa kutumia nguvu.”


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527