WAZIRI MKUU AITAKA TCU IVISAIDIE VYUO VIKUU BINAFSI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) itafute mbinu bora zaidi na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili.


“Tume itafute mbinu bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili. Ni wakati muafaka kwa Tume kujipambanua kwenye uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kwamba kazi kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kuvisaidia kutatua changamoto zinazovikabili,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo, (Jumatano, Julai 17, 2019) wakati akifungua maonesho ya 14 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yatafungwa Julai 20, mwaka huu.

Amesema Serikali inatambua kwamba vyuo vikuu binafsi ni washirika muhimu wa maendeleo ya sekta ndogo ya elimu ya juu nchini. “Naomba nieleweke vizuri kwamba hakuna mbadala wa elimu bora bali nasisitiza Tume ivisaidie vyuo vikuu kufikia viwango vinavyotakiwa na siyo kuwapunguzia viwango vya matakwa ya usajili,” amesema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu idadi ndogo ya wahitimu wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema takwimu za kimataifa za ushiriki wa elimu ya juu zinaonesha kwamba kufikia mwaka 2017 ni asilimia moja hadi tatu tu ya Watanzania kwa kila Watanzania 100 wenye umri chini ya miaka 25 wanapata elimu ya Chuo Kikuu.

“Idadi hii ni ndogo zaidi ya majirani zetu wa Kenya wenye asilimia nne, Zambia asilimia nne na Namibia asilimia 14. Bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya. Natoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iongeze jitihada na mikakati ya kuboresha uwiano huu ambao upo chini ikilinganishwa na majirani zetu,” alisisitiza.

Amesema ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata nafasi ya elimu ya juu, ni lazima tupange mikakati yetu kama nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi, ambao ni wadau wakubwa katika elimu ya juu. “Taarifa nilizonazo ni kwamba, kati ya wahitimu wote wa vyuo vikuu kwa mwaka, asilimia 25 wanatoka katika vyuo vikuu binafsi. Mchango huu si mdogo, na ningetamani uongezeke zaidi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapa changamoto wakuu wa vyuo vikuu nchini wabadilishe mtazamo wao juu ya upimaji wa ufanisi wa wahitimu na badala yake upimaji wao ujielekeze kwenye kutoa suluhisho na kubadilisha maisha ya Watanzania badala ya kutumia machapisho ya kitaaluma.

“Kipimo cha ufanisi katika taaluma ilikuwa ni machapisho ya kitaaluma, ambapo mengi ya hayo, jamii pana haifaidiki nayo. Sasa ni wakati mwafaka kutafakari iwapo kipimo hicho kinatosheleza. Kwa vyuo vikuu ambavyo mmehudhuria hapa leo, naomba niwape mtazamo tofauti. Kipimo cha ufanisi wa wanataaluma wa Tanzania, kuanzia sasa kinafaa kiwe ni kiasi gani taaluma yao inawafikia na kubadilisha maisha ya wananchi, na kiwango cha bidhaa na hatimiliki (patents) zilizozalishwa na kusajiliwa na wasomi wetu waliopo vyuo vikuu.”

Amesema matarajio ya Serikali ni kuona kwamba tafiti na vipimo vya ufanisi kwenye vyuo vikuu viwe ni kiasi gani vyuo hivyo vinatoa bidhaa mbalimbali za kuleta ajira pamoja na kukabiliana na matatizo ya kijamii. “Ningefurahi iwapo kuanzia sasa kipimo cha ufanisi wa vyuo vikuu vyetu iwe katika kupima jitihada za vyuo vyetu kuisaidia Serikali katika azma yake ya kufikia kwenye uchumi wa kati,” amesema.

“Huu ni wakati muafaka kuanza kupima ufanisi wa wakuu wa vyuo kwa kuangalia kiasi gani mazao ya Chuo Kikuu hicho yamewafikia wananchi na pia katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya Serikali, hasa mapinduzi ya viwanda,” amesisitiza.

Mapema, akielezea kuhusu maonesho hayo, Mwenyekiti wa TCU, Prof. Jacob Mtabaji aliwataka wahitimu wa kidato cha sita wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu, wasome kwa umakini mwongozo uliowekwa kwenye tovuti na wasikubali kupitia mawakala wanaodai kuwa wanaweza kufanya usajili kwa niaba yao. Pia aliwataka wazingatie kalenda ya udahili.

Akielezea changamoto za elimu ya juu nchini, Prof. Mtabaji alisema kuna uhaba wa wahadhiri wenye sifa stahiki katika vyuo vikuu vingi na akawaomba wakuu wa vyuo hivyo wawasomeshe wahadhiri katika ngazi mbalimbali ili wakirudi wajiunge na vyuo husika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa alisema taasisi 81 za elimu ya juu zimeshiriki maonesho hayo ambapo taasisi 15 ni za nje ya nchi na taasisi 66 ni za hapa nchini.

Akitoa shukrani, Mwenyekiti wa Kamati ya Watendaji Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki (CVCPT), Prof. Raphael Chibunda alisema anaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa uboreshwaji uliofanywa kwenye upatikanaji na upelekwaji kwa wakati wa fedha kutoka Bodi ya Mikopo. “Zamani, sauala hili hiloi likuwa ni chanzo cha migomo mingi vyuoni lakini kwa sasa limekwisha,” alisema.

Pia aliishukuru Serikali kwa kukubali kurudisha jukumu la udahili wa wanafunzi katika Seneti za Vyuo Vikuu kwani hapo nyuma lilikuwa sehemu ya mgogoro baina ya TCU na vyuo vikuu.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,       


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post