TAKUKURU DODOMA YAWANASA WATU WAWILI AKIWEMO MTENDAJI WA KATA KWA KOSA LA KUPOKEA RUSHWA MIL 4


Na.Faustine  Gimu Galafoni,Dodoma.
Taasisi ya kuzuia na    kupambana Rushwa ,TAKUKURU  kwa Mkoa wa  Dodoma  inawashikilia watu wawili akiwemo mtendaji wa kata kwa kosa la kupokea hongo ya Tsh.Milioni nne. 

Akizungumza na waandishi wa habari Leo Julai 24,2019  jijini Dodoma mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma  Bw.Sosthenes Kibwengo  amesema  mtendaji wa kata ya Mlowa Bwawani  wilaya ya Chamwino Bw.    Luis  Charles Pearson  na Mgambo  Bw.Josephat Ernest Msambili  wote wenye umri wa miaka [37]  walishikiliwa na TAKUKURU Kwa kosa la kushawishi  na kupokea hongo ya Tsh.Mil.4  kinyume  na kifungu cha  15[1]a  cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa  Na.11  Ya mwaka 2007. 


Watuhumiwa hao walimkamata na kumweka mahabusu ya kata  Bw.Samwel  Mabway   CHILULUMO ,mkazi wa kijiji cha WILIKO kilichopo kata ya MLOWA   BWAWANI Kutokana na ugomvi wa kifamilia . 


Wakati Chilulumo  akiwa yupo Mahabusu ndipo watuhumiwa   walipomtaka awape rushwa ya Tsh. Laki 6  ili wamwachie huru. 


Hata hivyo ,Bw.Chilulumo aliomba kupunguziwa  hadi kufikia Tsh.Laki nne na alipoomba atolewe mahabusu ili akatafute  fedha hizo watuhumiwa walikataa na kuamua kwenda kumtafuta mteja   wa mbuzi kumi[10] za Bw.Chilulumo zilizokuwa nyumbani kwake.

Aidha,Bw.Kibwengo  amesema uchunguzi wa TAKUKURU umethibitisha kuwa Mtuhumiwa Bw.Msambili alikwenda kutafuta mnunuzi wa Mbuzi hao na kumpeleka Mahabusu  alipokuwemo Bw.Chilulumo na baadaye kwenda nyumbani kuwakagua na akarudi tena mahabusu  ndipo walipokubaliana bei. 


Imethibitika kuwa mnunuzi huyo  alitoa  fedha hizo ambazo watuhumiwa walizipokea ndipo wakamtoa mahabusu na kumwachia huru  na TAKUKURU imekamilisha uchunguzi wa suala hilo na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani leo . 


Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma ametoa wito kwa watendaji wa kata,mitaa,vijiji kuenenda kulingana na maadili ya Kazi zao  na kujiepusha na  vitendo vya Rushwa  kwani havina nafasi katika serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe  Magufuli.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527