SERIKALI YAJIPANGA KUTUMIA TEKNOLOJIA SAHIHI ZA KILIMO ZINAZOENDANA NA MAHITAJI NA WAKATI

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Jitihada za kuongeza uzalishaji zinakuwa na mafanikio hafifu kutokana na kutotumia teknolojia sahihi zinazoendana na mahitaji na wakati; Mathalani, matumizi ya zana za kulimia ama zikiwa za mkono au zinazokokotwa na wanyamakazi au matrekta, zimekuwa zikisababisha mmomonyoko wa udongo hasa katika maeneo yasiyo tambarare na kusababisha upotevu mkubwa wa rutuba na kujengeka kwa jasi (hard pan).


Kwenye maeneo yenye mvua chache njia hizo za kilimo cha kukatua ardhi hazitunzi unyevu na kusababisha uzalishaji kuwa wa chini hasa pale panapokuwa na vipindi virefu vya ukame (dry spells) kama ilivyotokea msimu huu wa kilimo katika baadhi ya maeneo nchini ikiwemo Mkoa wa Dodoma.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 03 julai 2019 kwenye ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya kujadili kwa pamoja namna bora ya kuendeleza Kilimo Hifadhi nchini iliyofanyika katika ukumbi wa St. Gasper uliopo eneo la Kisasa, Jijini Dodoma.

Mhe Hasunga anasema kuwa kwa sababu hiyo basi, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kubadilisha mifumo inayotumiwa katika kuandaa mashamba ili kupata matokeo mazuri.

Amewashukuru Washirika wa Maendeleo (Development Partners) pamoja na Wadau wote wa Kilimo Hifadhi waliowezesha kufanikisha warsha hiyo muhimu wakiwemo African Conservation Tillage Network (ACTN), Canadian Food GrainBank (CFGB), Diocese of Central Tanganyika (DCT), na Conservation Farming Unit (CFU) –Tanzania.

Alisema juhudi hizo wanazofanya za kuendeleza Kilimo Hifadhi kwa kushirikiana na Serikali kwa maendeleo ya wakulima na Taifa kwa ujumla, ni sehemu ya mwelekeo wa kufikia Uchumi wa Viwanda kwa kukuza uzalishaji wenye tija.

Aliongeza kuwa jitihada hizo zinaendana na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013 na Programu ya  Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural Sector Development Programme - ASDP II) ambazo zinahimiza usimamizi endelevu wa matumizi bora ya maji na ardhi, kuongeza tija na faida katika uzalishaji, biashara na kuongeza thamani ya mazao na kuiwezesha Sekta katika uratibu, ufuatiliaji na tathmini.

Kadhalika Waziri Hasunga amesema kuwa ili kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo, Serikali imeongeza juhudi za kuwaunganisha wakulima na masoko, huduma za kifedha, usindikaji wa mazao na kuongeza thamani.

Alisema kuwa katika kutimiza azma hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Kilimo inaendelea Kuweka mazingira mazuri yanayovutia uzalishaji na uwekezaji, Kuimarisha mafunzo, Utafiti, ubunifu na uenezaji  wa teknolojia za kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na Kilimo Hifadhi na kuboresha Huduma za Ugani, Kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, uongezaji thamani ya mazao, kuimarisha ushirika, kuwaunganisha wakulima na masoko na huduma za fedha; na Kuhamasisha na kusimamia matumizi ya teknolojia za kisasa za kilimo ikiwemo teknolojia za kilimo hifadhi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe Mahamoud Mgimwa (Mb) alisema kuwa serikali inapaswa kujipanga vizuri kuendeleza Kilimo Hifadhi nchini kwa kufanya utafiti wa kina kwa utafiti ndio nguzo ya kilimo.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya mbegu zinaagizwa nje ya nchi hivyo aliiomba aserikali kuongeza Bajeti ya Wizara ya Kilimo hususani katika kuendeleza sekta ya mbegu.

Amesema Tanzania bado kuna tatizo kubwa la Masoko kwani wakulima wengi wanazalisha mazao yao lakini hawana mahali pakuyauza kwa bei nzuri huku wengine wakishindwa kusafirisha mzao yao kutokana na miundombinu kutoimarika kwa kiasi kikubwa. Kadhalika ameipongeza wizara ya Kilimo kwa kuanzisha mchakato wa mapitio ya sera ya kilimo ya 56mwaka 2013 itakayopelekea kuwa na sheria mpya ya Kilimo.

Awali akitoa salamu za wizara ya Kilimo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua warsha hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe alisema kuwa Lengo la warsha hiyo ni kuwawezesha washiriki kupata uzoefu na kufahamu juhudi na matokeo ya kazi za kuendeleza kilimo hifadhi zinazofanyika nchini na kuweka mpango utakounganisha, kuratibu na kusimamia shughuli za kuendeleza matumizi bora na endelevu za teknolojia za kilimo hifadhi nchini.

Alisema kuwa matumizi ya kilimo cha kisasa (smart agriculture)  ikiwa ni pamoja na kilimo hifadhi ni nguzo katika kuendeleza kilimo nchini kwa kongeza tija, kuboresha ardhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa katika maeneo yanayopata mvua chache.

Mhandisi Mtigumwe alisema kuwa Katika miaka ya hivi karibuni, matumizi ya teknolojia ya kilimo hifadhi yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka. Tathmini zilizofanywa na Wizara zinaonyesha kuwa karibu hekta 40,000 nchini zinalimwa kwa kutumia  kilimo hifadhi na matokeo yanaonyesha kuwa mavuno (yields) wanayopata wakulima kutoka kwenye mashamba ya kilimo hifadhi ni mazuri hata wakati wa mvua chache.

Aliongeza kuwa Katika kipindi hiki, ambacho Serikali inajitahidi kuongeza miundo mbinu ya umwagiliaji na kuongeza matumizi ya mbolea za viwandani kwa gharama kubwa ili kuongeza tija na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, matumizi ya teknolojia ya kilimo hifadhi ni njia mbadala ya kufikia malengo hayo kwa haraka na kwa gharama nafuu.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527