SERIKALI YAJIPANGA KUBORESHA MIUNDOMBINU KWENYE KIMONDO CHA MBOZI


Serikali imeahidi kujenga miundombinu ya kudumu katika Kituo cha  Kimondo Mbozi kwa ajili ya maonesho ili kuhamasisha na kukuza utalii kwa mikoa ya Nyanda za juu Kusini.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati alipokuwa akifunga Maadhimisho ya Siku ya Kimondo Duniani yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu katika kijiji cha Ndolezi mkoani Songwe.

Amesema shabaha ya serikali ya awamu ya tano ni kukuza na kuendeleza Utalii Kusini.


Ametaja  miundombinu hiyo itakayojengwa kuwa ni mabanda ya kudumu, viwanja vya michezo,  jengo la kupokelea watalii hali itakayosaidia  Kituo hicho kuwa na miundombinu bora ya utalii katika ukanda huo.

Mbali na miundombinu hiyo amesema wataangalia uwezekano wa kulipa fidia kwa wananchi ili kuongeza ukubwa wa eneo litakalotumika kwa ajili ya shughuli za kiutalii kama vile kuanzisha bustani ya wanyamapori hai.

Mhe.Kanyasu amesema mkakati wa Serikali ni kuyafanya  Maonesho hayo  yawe ya kudumu na yenye hadhi ya kitaifa ambapo baada ya Halmashauri kulipima eneo hilo Taasisi za Wizara zitashiriki katika uwekaji wa miundombinu hiyo.

Aidha, Amesema  Kwa uwepo wa Kimondo hicho ni fursa kwa wananchi kuweza kujipatia kipato kufuatia watalii kutembelea kituo hicho.

Amesema Wizara yake  imelikabidhi eneo hilo la Kimondo kwa Mamlaka ya Eneo la Ngorogoro( NCAA) ili kuchagiza utalii na  jukumu la msingi la NCAA ni kuhakikisha wanatengeneza miundombinu bora kwa ajili ya Utalii.

Tunataka eneo hili la Kimondo, Mtalii yeyote atayefika aweze kuona ngoma za asili pamoja na vitu vingine vya kiutamaduni vitakavyomvutia ili aweze kuona kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Nicodemus  Mwenga mesema wamejipanga ipasavyo kuhamasisha jamii kuanza kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio Nyanda za Kusini.

Katika Maadhimisho hayo Wakuu wa mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na  Makatibu Tawala wameungana kwa pamoja kutangaza vivutio vya utalii Kwa pamoja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post