SERIKALI YAANZISHA UTALII WA FUKWE ZIWA VICTORIA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kigwangala amesema wameanzisha utalii wa fukwe katika ziwa Viktoria na kwamba tayari Mamlaka ya hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) inajenga kivuko kitakachokuwa na uwezo wa kupakia magari manne hadi sita na abiria wasiopungua 100.


Kigwangala ameyasema hayo jana Jumanne Julai 9, wilayani Chato mkoani Geita katika hafla ya uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,702 ambapo amesema kuwa kuna wanyama waliokuwepo katika hifadhi hiyo na baadae wakatoweka hivyo watafanya jitihada za kuwarudisha katika makazi yao ya asili.

“Katika mapori haya kulikuwa na Faru lakini walitoweka na tunajua aina ya Faru waliokuwepo hapa hivyo tutafanya jitihada za kuwarudisha katika makazi yao, pia tunatarajia kupokea faru 10 wenye asili ya Tanzania kutoka nchi za nje kuja kuongeza idadi ya faru katika nchi yetu,” amesema.

Aidha amesema kuwa walipopandisha hadhi mapori hayo uwindaji umekoma na matumizi yatabadilika na kwamba kiwango cha ulinzi na uhifadhi kitaongezeka kwa kiwango cha juu.

“Katika kipindi ambacho uvamizi ulikuwa umetamalaki wanyama wengi walitoweka lakini tangu tumepandisha hadhi mapori haya idadi imeanza kurudi,” amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527