RAIS MSTAAFU MWINYI AUPONDA WARAKA WA KINANA NA MAKAMBA ....'NI UTOTO'


Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, amesema kitendo cha makatibu wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba kuandika waraka kuhusu hali ya kisiasa nchini, ni utoto.

Kauli hiyo ameitoa ikiwa zimepita siku chache tangu viongozi hao walipoandika waraka kwenda Baraza la Viongozi Wastaafu na kuzua gumzo kwa viongozi na wananchi wa kada mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa Mwinyi hakubaliani na jambo hilo.

“Kuhusu waraka ulioandikwa na makatibu wakuu wastaafu, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba kwenda kwa Baraza la Viongozi Wastaafu, ni utoto,” alisema Mwinyi.

Alipongeza majibu yaliyotolewa na Katibu wa Baraza hilo, Pius Msekwa na kusema walioandika waraka huo wameshindwa kufuata katiba na taratibu za chama.

“Viongozi wastaafu hawawezi kupoteza muda wao kwa masuala ya kitoto,” alisema.

Aliwataka Watanzania kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya za kuleta maendeleo kwa muda mfupi.

Alisema ukiondoa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, viongozi wengine waliofuata akiwemo yeye, wamefanya juhudi za kuipeleka nchi mbele, lakini kasi ya Rais Magufuli ni kubwa zaidi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527