NEC YATANGAZA UCHAGUZI JIMBO LA TUNDU LISSU KUFANYIKA MWEZI HUU

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Singida Mashariki, mkoani Singida utakaofanyika Julai 31, mwaka huu.


Akitangaza hatua hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,  Jaji Semistocles Kaijage amesema ratiba inatokana na barua ya Spika inayoeleza kuwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Tundu Lissu amepoteza sifa ya kuwa Mbunge kutokana na kushindwa kuwasilisha kwa Spika tamko la mali na madeni na kushindwa kuhudhuria mikutano saba mfululizo bila ruhusa ya Spika.

“Tumezingatia  matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, kutoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki,” amesema.

Jaji Kaijage amesema, fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya Julai 13 hadi 18 mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika Julai  18, na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30 na siku ya uchaguzi itakuwa ni Julai 31, mwaka huu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527