NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHE. CONSTANTINE KANYASU AONYA WAHARIBIFU WA MISITU


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amesema Tanzania kwa mwaka mmoja inateketeza takribani hekta 400,000 za misitu ambapo endapo hali hii  itaachwa hivyo Misitu iliyopo nchini itaisha baada ya miaka 12

Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu amesema Wizara yake itaendelea kulinda misitu hiyo kwa nguvu zake zote ili kuweza kuinusuru.

Hayo ameyasema mkoani Geita  wakati alipokuwa akizungumza na Wachimbaji Wadogo wa madini kwenye mkutano uliolenga kutoa elimu kwa Wachimbaji hao kuhusu  umuhimu wa kurasimisha mali.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhe.Kanyasu amesema shughuli za uchimbaji madini zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa katika uteketezaji wa misitu hiyo.

Amesema Wachimbaji walio wengi wamekuwa ni watu wa kuhama hama na kila mahali wanapohisi kuna madini wamekuwa wakifyeka misitu bila kujali athari zake..

Ameongeza kuwa kwa vile Wachimbaji hao wamekuwa wakifyeka misitu hiyo katika maeneo  makubwa hata baada ya kumaliza uchimbaji huo hushindwa kupanda miti mingine.

Amewaeleza kuwa madhara yake ni makubwa na  kama hali hiyo itaendelea kwa vile mara baada ya misitu hiyo kuisha mvua hazitaweza kunyesha na hali ya maisha itakuwa ngumu sana.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka Wananchi wanaokata miti iwe yao walioyaipanda uwe mwembe au mti wa aina yeyote wafuate taratibu za kupata kibali kwa Maafisa misitu au wenyeviti wa maeneo husika.

Amesema kwa wale  wanaokata miti hiyo bila kupata kibali kwa mamlaka husika, Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Stanlaus  Nyongo amewataka Wachimbaji hao kufuata sheria pale wanapohisi uwepo wa madini katika maeneo ya  Hifadhi

Amewataka watoe taarifa kwa Wamiliki wa Hifadhi kwa ajili ya kupata idhini badala ya kuanza kuvamiwa maeneo hayo kwa kuanza kufyeka misitu.

Naye, Hamisi Abdala aliyejitambulisha kama Mchimbaji mdogo amesema atakuwa Balozi kwa Wenzake kwa kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kulinda misitu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post