NAIBU SPIKA ATAKA MISINGI YA UTAFITI KUFUATWA KATIKA UCHAPISHAJI NA UTANGAZAJI WA TAARIFA


NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amesema misingi ya utafiti ni jambo muhimu na la msingi litakalopaswa kuzingatiwa katika uchapishaji na  utangazaji wa taarifa mbalimbali ili kuweza kulinda misingi ya amani iliyopo nchini.


Akizungumza leo Jumanne (Julai 9, 2019) Jijini Dar es Salaam katika Kongamano maalum la siku ya Amani lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF), Dkt. Tulia alisema uchapishaji na utangazaji wa taarifa yoyote haina budi kuwa na tija katika taifa.

Dkt. Tulia alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na utamaduni uliozoeleka wa kutangaza na kuchapisha taarifa mbalimbali katika jamii kupitia vyombo vya habari pasipo na kuzingatiwa kwa misingi ya utafiti hatua inayoweza kuleta migongano isiyo na tija kwa taifa.

“Serikali ya Awamu ya Tano tunaona inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo mradi wa umeme katika Mto Rufiji, sni wajibu wetu kulinda misingi ya amani iliyopo ili tuone matunda ya miradi hii katika nchi yetu” alisema Tulia.

Aidha Dkt. Tulia alisema ni wajibu wa misingi ya utafiti ikazingtiwa katika taaluma mbalimbali ikiwemo ya uandishi wa habari kwani wapo baadhi ya watu wanaofikiri kuwa wanaweza kuandika na kutangaza habari pasipo na kusomea taaluma hiyo, jambo ambalo si la kweli kwa kuwa uandishi wa habari ni taaluma nyeti na muhimu kama zilivyo taaluma nyingine.

Aliongeza kuwa ni wajibu wa Watanzania wote kusoma vitabu mbalimbali vilivyoandikwa na waasisi wa taifa vikiwemo vitabu vya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambavyo vimekuwa na wingi wa maarifa na  maelekezo yanayopaswa kuzingatiwa ili kuweza kujenga taifa lenye umoja, upendo na mshikamano.

Naye Mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano Zanzibar, Imane Duwe alisema mfumo wa soko huria nchini yameleta mabadiliko makubwa katika tansia ya habari na mawasiliano ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii, ambayo imekuwa imeleta hamasa kubwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo vijana.

“Hapo awali mwandishi wa habari alipokuwa akitumwa kazi na mhariri wake ni lazima arudi na atoe taarifa kwa mkuu wake pamoja na habari au taarifa hiyo kuweza kufanyiwa uhariri kabla ya kuchapishwa na kutangazwa lakini kwa sasa hali ni tofauti kidogo, kwani tukio lolote linaweza kutumwa wakati huo huo kupitia vyombo vya kisasa zaidi vya mawasiliano” alisema.

Aliongeza kuwa vyombo vya habari vya zamani ikiwemo Magazeti, Redio na Televisheni kwa sasa navyo vimeingia katika ushindani mkubwa wa soko kwani kwa upande wao pia wameanzisha mitandao mbalimbali ya kijamii ili kuweza kuwa na njia za kisasa zaidi za mawasiliano.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema ni wajibu wa Viongozi na Watanzania wajenge utamaduni wa kuheshimu tunu na misingi mikuu ya amani nchini ikiwemo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, misingi ya Azimio la Arusha ambayo iliasisiwa na Hayati Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Nyerere.

Aidha aliongeza kuwa ili kuweza kujenga Taifa lenye misingi bora ya amani ni wajibu wa Serikali kupitia Viongozi kuwa na  matumizi na usimamizi bora wa rasilimali za taifa na kuhakikisha zinawanufaisha  wananchi wote pamoja na kuweka misingi imara katika ulinzi rasilimali hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Amani Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema Tanzania inaweza kufikia na kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda iwapo Viongozi wataweka mkazo katika usimamizi wa rasilimali watu yenye kutambua umuhimu wa kulinda amani, weledi, uzalendo na kujiamini.

“Moja ya Nguzo muhimu katika kufikia uchumi wa viwanda ni mfanyakazi, hivyo ni wajibu kila mwenye dhamana hiyo kutimiza wajibu wake huku akiogopa kufanya vitendo vya ufisadi kwani hata katika vitabu takatifu vimezungumzia ufisadi ni jambo baya sana”  alisema Sheikh Salum.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527