AUAWA KWA KUKATWA SHINGO BAADA YA KUFUMANIWA NA MPENZI WA MTU KICHAKANI

Kijana Fadhili Abdallah Mkunguja {23} mkazi wa Kijiji cha Ruchemi, Kata na Tarafa ya Milola, Mkoa wa Lindi, amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa kukatwa shingoni na kitu chenye ncha kali na mwenzake aitwae Issa Khalifa Mtumwa (20) katika ugomvi uliotokana na wivu wa kimapenzi.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, wameeleza kuwa mauaji hayo yamefanyika wakati wananchi kijijini hapo wakiwa katika sherehe za ngoma ya unyago, ambapo wamesema marehemu alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mchumba wa Issa Khalifa, aitwae Hawa Hamadi {15} na kufanikiwa kupata nae Mtoto mmoja.

"Issa na huyo Hawa ni mtu na mchumba wake, wanaishi nyumba moja kupika na kupakua na wamefanikiwa kupata mtoto wao mmoja", ameeleza mmoja wa mashuhuda ambao hawakutaka jina lake kutajwa.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ruchemi, Ally Mussa Mkalola, amekiri kuwepo kwa taarifa hizo na yeye akizipokea kutoka kwa wasamalia wema kuwa mchumba wa Hawa amekutwa akiwa na Fadhili Abdallah wakielekea kichakani.

Mkalola amesema taarifa hiyo ilimfanya Issa kupandwa na hasira na kuamua kuwafuatilia huku akiwa ameshika panga mkononi, kwa ajili ya kwenda kumshambulia Fadhili ambaye kwa wakati huo alidaiwa kuwa na mchumba wake.

"Kitendo cha kumkuta Fadhili ameketi na mchumba wake pale chini ya mti, hakuuliza alichokifanya ni kumshambulia shingoni yule mgoni wake, huku yule msichana akitimua mbio kuelekea nyumbani kwao", amesema Mkalola.

Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, ACP Prodansiana Protas alipoulizwa kuhusiana na mauaji hayo, amethibitisha kutokea na kueleza kuwa wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa Issa Khalifa, ili sheria ichukue mkondo wake.
Chanzo - EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post