LUGOLA ASEMA POLISI WANAOSHIRIKIANA NA MAFISADI KUDHULUMU ARDHI YA WANANCHI MASKINI, DAWA YAO IMEIVA


Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA)
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema baadhi ya polisi wasiokuwa waaminifu nchini wanaoshirikiana na mafisadi kudhulumu ardhi ya wananchi maskini, sasa dawa yao imeiva. 


Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Haruzale, Kata ya Nyamihyolo, Jimbo la Mwibara, Bunda akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo jimboni mwake, Lugola amesema amepokea malalamiko mengi ya ardhi katika jimbo lake na sehemu mbalimbali nchini.

Amesema mafisadi wa ardhi hukimbilia kufungua kesi vituoni wakilazimisha kwa kutumia fedha ardhi iwe mali yao wakiwatumia polisi wasiokuwa waaminifu ili kufanikisha matwaka yao.

“Haiwezekani tabia hii ikachekewachekewa na kuonekana ni kawaida, nimekemea sana katika mikutano yangu hapa Mwibara na sehemu zinginezo hapa nchini, nitahakikisha napambana na mafisadi pamoja na polisi hao wasiokuwa waaminifu,” alisema Lugola.

Waziri Lugola alisema kila kukicha anapata malalamiko mengi kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa mafisadi wanaendelea kuwaonea wananchi maskini kwa kupora ardhi wakidai wao ndio wamiliki halali. Aliongeza kuwa, utumia polisi wasiokua waaminifu kuwakandamiza wananchi ambao hawana nguvu ya kifedha na kufanikiwa kudhulumu ardhi zao.

“Dawa yao ilikuwa jikoni, sasa imeiva, siwezi mwangusha Mheshimwa Rais Dkt. John Magufuli, Serikali hii haichezewi hata siku moja, sasa nitawashughulikia ipasavyo,” alisema Lugola.

Aidha, Lugola aliwataka wananchi wa Mwibara kuhifadhi vyakula vizuri ili kuepusha janga la njaa kwa hapo baadaye na kusababisha wananchi kuja kuteseka kwa ukosefu wa vyakula na kusababisha mateso katika familia. 


“Tutunzeni vyakula vyetu, msitumie hovyo, kuweni makini na matumizi ya vyakula, sitaki nije kuona mnateseka na njaa, hakikisheni mnatunza vyakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ogopeni njaa kama ukoma,” alisema Lugola. 


Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, alifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo akikagua madarasa ya shule ya msingi pamoja na zahanati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527