JAMAL MALINZI NA KATIBU WAKE SELESTINE MWESIGWA WAKUTWA NA KESI YA KUJIBU


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewakuta na kesi ya kujibu aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu(TFF), Jamal Malinzi na Katibu wake Selestine Mwesigwa katika mashtaka 20 kati ya 30 ikiwemo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha.


Wengine waliokutwa na kesi ya kujibu ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, na Karani Flora Rauya huku Meneja wa TFF, Mariam Zayumba akiachiwa huru.

Uamuzi huo umetolewa jana Jumanne Julai 23, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na Jamhuri.

Hakimu Kasonde alisema mashtaka ambayo washtakiwa wameonakana hawana kesi ya kujibu, upande wa Jamhuri umeshindwa kuonesha kama washtakiwa wana kesi ya kujitetea.

Mahakama iliwafahamisha haki zao washtakiwa kwamba wanaruhusiwa kujitetea wenyewe kwa kiapo ama kuita mtu yoyote kama mashahidi wao.

Pia walifahamishwa kwamba wanayohaki ya kunyamaza kimya lakini kwa kufanya hivyo mahakama itaamini kwamba ushahidi uliotolewa na Jamhuri ni sahihi.

Washtakiwa walikubali kujitetea kwa kiapo na watakuwa na mashahidi ambapo wataanza kujitetea Agosti 6 mwaka huu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Katibu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 20 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017. Ambapo Meneja wa Ofisi TFF, Miriam Zayumba ameachiwa huru.

 Kesi imeahirishwa hadi Agosti 6, mwaka huu kwa ajili ya kuanza kujitetea utetezi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527