'FACEAPP' MITANDAO INAVYODUKUA TAARIFA ZAKO HUKU UKICHEKELEA....'KIJANA ANAONEKANA MZEE'


Leah Mushi,Mtanzania Dar es Salaam
Miongoni mwa vitu vinavyosambaa mitandaoni kwa sasa ni hii ‘Application’ ya ‘FaceApp’ ambayo ina uwezo wa kubadilisha picha yako na kukuonesha ukiwa mzee.
Na kwa siku chache App hii imejizolea umaarufu kwa watu wengi kuitumia (nikiri tu mimi si mmoja wao).

Kutokana na umaarufu huo tayari wataalamu wa masuala ya mitandao na teknolojia wameanza kuinyooshea kidole kuwa inachukua taarifa za watu na kwamba si salama na inasemekana imebuniwa huko nchini Urusi hivyo kuwasihi watu kuwa makini na pengine wasiitumie kabisa.

Pengine ni kweli wayasemayo lakini ni mtandao gani wa kijamii usiochukua taarifa zako? Kwanini wauseme huu na wala wasiseme mingine yote?
Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliwahi kusema; ukitaka kula sharti na wewe ukubali kuliwa kidogo na ndiyo ilivyo kwa mitandao hii ya kijamii.
Tunaona tunaingia bure na kutuma (post) tutakavyo, lakini wamiliki wake wana taarifa zetu (wewe ni nani, upo wapi, unapenda kuperuzi vitu gani, unatumia muda kiasi gani mtandaoni, jinsia yako n.k.) orodha ni ndefu. Na taarifa hizi ndiyo huziuza kwa watu wa matangazo na ndiyo maana utaona kitu unachopost basi watakuwa wanakupa matangazo (sponsored ads) zinazofanania na kitu unachoperuzi kwa wakati huo.
Kwa mfano; mimi binafsi tangu nianze kupost binti yangu akicheza tennis baasi matangazo na kurasa (page za tennis) zimekuwa zikija kwangu hivyo hivyo kwa wewe jaribu kupost kitu chochote kwa wiki moja mfululizo utaona mwelekeo wa matangazo yatakayokuja kwako.
Pengine ni siasa za kibiashara za haya mataifa makubwa huko duniani kuchafuliana lakini pia hii itukumbushe kuwa tusikurupukie kila kinachotokea na kusambaa kwenye mitandao (online trending), maana huwezi jua mwisho wake.
Mwisho nikutoe hofu kuwa hata usipoingia mtandaoni taarifa zako zitachukuliwa tu yaani huo ndio ukweli.

Wangapi mnatumiwa matangazo na kampuni za simu? Hiyo ndiyo miongoni mwa namna za kujipatia fedha kwa hayo makampuni .
Hivyo basi ndugu yangu tumia mitandao kwa akili bora kuwa mshamba kuliko limbukeni lakini pia usichukulie maisha ‘very serious’ (kwa umakini sana), jiachie, ndiyo maana inaitwa ‘social’ yaani kijamii zaidi usiogope unavyoliwa taratibu taratibu.
Huko Facebook ndiyo mnaliwa kupita maelezo, huwa nikiona yale matangazo yanayouliza “Leah unajua maana yake? Utakuwa wapi baada ya miaka 10? Utaolewa na mwanamume gani?” Wote wale wanakusanya data zenu.
Kwa muda mrefu nchini Marekani imekuwa ikichukua taarifa zako maana ndiyo haya makampuni yalipo, sasa hivi Urusi nayo ina taarifa zako kwa hizo FaceApp.
Sasa yajayo yanafurahisha maana tunaambiwa kitu cha ‘5G’ yenye uwezo wa kupakua filamu ya zaidi ya saa moja kwa sekunde chache na hiyo inasemekana China ndiyo inaharakisha kuitoa kwa dunia.
Ndugu yangu huna pa kukimbilia, wewe tumia tu mitandao kwa heshima na adabu na tulia uliwe kidogo kidogo!
Mwandishi wa makala haya ni Mtaalamu na Mkufunzi wa Dijitali.
+255 713 142 101
CHANZO - MTANZANIA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527