Deni La Tshs Bil. 7 Lawaweka Pabaya Wadaiwa Sugu Wa NARCO

Na. Edward Kondela
Serikali imesema wadaiwa wote waliowekeza katika ranchi za taifa zinazomilikiwa na Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) walipe madeni yao kabla haijachukua hatua ya kuwanyang’anya maeneo na kuwafikisha mahakamani.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema hayo jijini Dodoma katika ofisi za makao makuu ya NARCO wakati akizungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu 111 katika ranchi za taifa zilizopo maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kulisha mifugo yao ambapo hadi sasa wanadaiwa Tshs Bilioni Saba.

“Lipeni bila shuruti, ahadi yangu kwenu mkifanya majukumu yenu ofisi yangu itawapatia ushirikiano wa kutosha, kwa wale ambao hawalipi watakuwa wamepoteza sifa za kuwa wawekezaji na siyo kwamba itaishia hapo tutachukua hatua za kisheria na watalipa deni ili kusudi watanzania wengine wawekeze ambao wanaweza kulipa hela ya serikali, hulipi nitakuondoa tena nitakufunga.” amesema Prof. Gabriel

Prof. Gabriel ameitaka NARCO kuhakikisha makampuni matano ambayo yanadaiwa fedha nyingi zaidi zinazokaribia tshs Bilioni Moja, yalipe fedha hizo ili kuiwezesha NARCO iweze kufanya shughuli zake na kuboresha ranchi inazozisimamia.

Katibu mkuu huyo ameitaka pia NARCO kuwekeza katika ranchi zake ili wawekezaji waweze kupata huduma mbalimbali muhimu kwa ajili ya mifugo yao yakiwemo maji na malisho pamoja na kuboreha njia za mawasaliano na wawekezaji, kutengeneza mpango wa uwekezaji na mikakati ya kiusalama.

Aidha Prof. Gabriel ameutaka uongozi wa Umoja wa Wawekezaji wa Ranchi za Taifa (UWARATA) kufanya kazi kwa kufuata misingi ya kisheria ikiwemo kusajili chama chao ili kiwe na nguvu ya kusimamia wanachama wao katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria za nchi na kuwa daraja la mawasiliano kati ya Wizara ya mifugo na Uvuvi na NARCO.

Akizungumza kuhusu deni la tshs Bilioni Saba wanalowadai wawekezaji, kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu wa Narco Prof. Philemon Wambura, Meneja Masoko wa NARCO Bw. Emmanuel Mzava amesema deni hilo limedumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa na wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kuwasiliana na wawekezaji ili waweze kulipa na katika kikao hicho kuweka mkakati wa kulipwa deni hilo.

“Baada ya kufanya kikao na katibu mkuu sisi watendaji tuliobaki hapa pamoja na wawekezaji katika vitalu vilivyopo katika ranchi za taifa, miongoni mwa mambo tunayofanya ni kuwekeana sasa kama makubaliano madogo ambayo yameandaliwa kwamba mwekezaji tunamsomea deni lake na tunakubaliana lini analipa deni lake.” Amesema Bw. Mzava.

Nao baadhi ya wawekezaji waliofika katika kikao hicho wamesema kimekuwa na manufaa makubwa kwao ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili na kuwa na misingi mizuri ya kuendelea kumiliki vitalu walivyopatiwa na kulisha mifugo yao kwa kufuata sheria za nchi.

Kikao cha katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, uongozi wa Kampouni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) na wanachama wa Umoja wa Wawekezaji wa Ranchi za Taifa (UWARATA), kimefanyika ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina kuutaka uongozi wa NARCO kubadilika na kutumia maeneo yake kwa ajili ya kuwekeza na kupata faida ili iweze kujiendesha na kutoa gawio serikalini.

Wanachama hao walioshiriki kikao hicho wanatoka katika vitalu 111 vilivyopo katika ranchi za Kagoma, Kikulula, Mabale na Kitengule zilizopo Mkoani Kagera, ranchi zingine ni Uvinza, Usangu na Kalambo zilizopo Nyanda za juu Kusini na ranchi za Mkata, Mzeri, Dakawa zilizopo Mashariki na Pwani.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post