KATIBU MKUU WA CCM ASEMA KUNA MTU ANATAKA KUIVURUGA CCM

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema ndani ya chama hicho tawala nchini Tanzania kuna kocha aliyeanzisha tabia ya kukivuruga, akibainisha kuwa hawezi kufanikiwa.

Dk Bashiru ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 23, 2019 mkoani Dodoma wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho mkoani humo alikokwenda kuzindua mradi wa vibanda vya biashara.

Bila kumtaja mtu jina, amesema kocha huyo ameanza mchezo wa kitoto kwa lengo la kukivuruga chama jambo linalovifanya vyama vya upinzani kudandia hoja yake.

Ametoa kauli hiyo wakati ambao makada mbalimbali wa CCM wamejitokeza kulaani kitendo cha makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kumuandikia barua katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho wakilalamika kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Makada ambao tayari wamejitokeza kuzungumzia barua hiyo ni wabunge; Joseph Kasheku ‘Musukuma’ (Geita), Nape Nnauye (Mtama), James Millya (Simanjiro), Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ (Mtera) na Hussein Bashe (Nzega Mjini) ambaye jana aliapishwa kuwa naibu waziri wa kilimo.

Na Habel Chidawali, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527