WANUNUZI WATAKIWA KUNUNUA PAMBA KWA BEI ELEKEZI

Na Stella Kalinga, Simiyu

Waziri wa Kilimo amewaomba wanunuzi wa pamba waliopewa leseni na Bodi ya pamba wanunue pamba kwa wakulima kwa bei elekezi ya shilingi 1200 kama ilivyopangwa na kukubaliwa katika kikao cha wadau wa pamba mwezi Mei, 2019 jijini Mwanza.

Waziri Hasunga ameyasema hayo Juni 15, 2019 wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu wakati alipotembelea viwanda vya kuchambua pamba, vituo vya kununulia pamba na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.

“Naomba nitumie nafasi kuwaomba wanunuzi wa pamba wenye nia njema na nchi hii waliopewa leseni na Bodi ya Pamba waje kununua pamba kwa wakulima, bei elekezi ya mwaka huu ni shilingi 1200”-alisema Waziri Hasunga.

Aidha, Waziri Hasunga amevitaka vyama vya ushirika vya msingi kuzikagua mizani kwani itakapobainika kufanyika uchakachuaji wakati wa kupima hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria, huku akiwahakikishia wakulima kuwa changamoto zote zilizobainishwa na wakulima katika msimu wa 2018/2019 zitafanyiwa kazi.

Mkulima wa Pamba kutoka Luguru wilayani Itilima, Bw. Ngusa Lutenganeja ameishauri Serikali kupanga bei ya pamba wakati wa maandalizi ya msimu ili wakulima walime wakiwa wanafahamu bei na maandalizi ya fedha yafanyike mapema wakulima wasikopwe pamba yao.

Kwa upande wake Mnunuzi wa pamba ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Itilima, Mhe. Njalu Silanga amesema imani yake ni kwamba Serikali itasimamia na kuhakikisha pamba ya wakulima inanunuliwa kwa bei elekezi ya shilingi 1200/= na wananchi wanapata fedha zao kwa wakati.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema mkoa wa Simiyu una viwanda vingi vya kuchambua pamba, ambapo ameshauri kuwa ili kuliongezea thamani zao la pamba Wizara ya Kilimo kwa  kushirikiana na wadau wengine kuona uwezekano wa kujenga kiwanda cha  kutengeneza nguo  kwa kuwa uhakika wa soko la bidhaa zitakazotengenezwa upo.

Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa pamba nchini (TCA), Bw. Boaz Ogola ametoa wito kwa Wanunuzi wa pamba kuunga mkono juhudi za Serikali katika viwanda kwa kuwekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya pamba ili tusitegemee soko nje ambalo linayumba.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post