WAKULIMA MKOANI MBEYA WALALAMIKIA MIFUGO KUINGIA MASHAMBANI


Na Amiri kilagalila
 Licha ya serikali  kukemea vitendo vya mapigano baina ya wafugaji na wakulima nchini, wakazi wa kijiji cha Ipwani wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameiomba serikali kuwakamata wafugaji wanaoingiza mifugo ya ng’ombe kwenye mashamba ya mpunga wanayovuna hivi sasa, huku wafugaji hao wakituhumiwa kuwapiga na kuwapa ulemavu wa kudumu.

Kijiji cha Ipwani kinachopakana na wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe kinasifika kwa kulima zao la mpunga kwa wingi, hata hivyo hofu imewakumba wakazi wa kijiji hicho kilichopo wilayani Mbarali mkoani Mbeya kutokana na vitendo vinavyofanywa na wafugaji kabila la wasukuma kuingiza idadi kubwa ya ng’ombe katika mashamba ya wakulima wa mpunga , kitendo ambacho   baadhi ya wakazi waliopigwa na kupata ulemavu wamekilaani kitendo hicho na  kuziomba mamlaka kuingilia kati.

“kuna siku niliondoka na kijana wangu kwenda shambani kupiga mpunga lakini wakatokea wafugaji hawa wa kabila la kisukuma wakawa wanataka kulisha mpunga na hizo ng’ombe zao nilivyojaribu kuwazuia wakaanza kunishambulia na kunivunja mkono”alisema Juliana Mkupala mmoja wa wakazi wa Ipwani

Viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Ipwani  wamekiri kutokea mgogoro huo huku tangazo likitolewa na afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ipwani kwa wafugaji kuepuka kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na watatozwa faini ya shilingi laki moja mifugo ikipatikana mashambani

“Hii changamoto ipo,wafugaji wamekuwa wakileta ugomvi lakini kama ofisi ya kijiji huwa hatuna mamlaka ya kuweza kusuluhisha mfano jambo la kupigwa kwa hiyo huwa tunawaandikia barua ya kwenda ngazi za juu,kwenye kituo cha polisi ili washughulikiwe”alisema Yasinta Pugili afisa mtendaji wa kijiji.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post