DKT. KIJAZI ASHINDA KWA KISHINDO NAFASI YA UMAKAMU WA TATU WA RAIS WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)


Na: Monica Mutoni. Geneva
Kwa mara nyingine Tanzania imeingia katika historia ya kimataifa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na mwakilishi wa kudumu Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuibuka mshindi wa nafasi ya umakamu wa tatu wa Rais wa WMO. Dkt. Kijazi anachukua nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2019-2022 akiwa mwanamke wa kwanza na mjumbe wa kwanza kutoka nchi zinazoendelea kushika nafasi hiyo. Dkt. Kijazi atakuwa na majukumu makubwa ya kumsaidia Rais kuongoza shirika hilo katika kutekeleza majukumu yenye tija kwa wanachama wake ikiwemo Tanzania


Akizungumzia ushindi wake mbele ya wapiga kura wa mkutano wa 18 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na wajumbe waalikwa, Dkt. Kijazi alitoa shukrani zake za dhati kwa wote waliomwamini na kumuunga mkono hadi kufika kupata nafasi hiyo na kuahidi kuitumika nafasi hiyo kwa weledi wa hali ya juu ili kufikia malengo ya shirika hilo.

‘ Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wote waliokuwa pamoja na mimi kwa kuniunga mkono na kunichagua kwa kura zote, naahidi kuitumikia nafasi hii kwa weledi mkubwa na kuhakikisha WMO inafikia malengo yake’. Alisema Dkt Kijazi

Akizungumzia ushundi huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Atashasta Nditiye alisema ni heshima kubwa sana kwa nchi, Wizara inampongeza sana Dkt. Kijazi na kuamini kuwa ataiwakilisha nchi vizuri, aidha alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano aliouonesha kwa kukubali Tanzania kuwakilishwa na Dkt. Kijazi ambapo kwa jitihada zake katika kuboresha sekta ya hali ya hewa kumeendelea kuiletea sifa nchi kwa ujumla

Kwa upande wa Kaimu Balozi, Ubalozi wa Kuduma Umoja wa Mataifa, Geneva Ndugu. Robert Kahendaguza alisema kuwa ushindi wa Dkt. Kijazi ni kielelezo cha umadhubuti wa kidiplomasia ya Tanzania na sifa zake binafsi ikiwemo uzoefu wa muda mrefu na elimu ya ngazi ya juu katika nyanja ya sayansi ya hali ya hewa, aidha aliongeza kuwa sababu za sifa hizo ziliupunguzia ubalozi kazi ya kumnadi na hata kuwa rahisi kuishawishi nchi ya Sudan kuondoa mgombea wao na hivyo kumfanya Dkt. Kijazi kuwa mgombea pekee katika uchaguzi huo.

Uchaguzi wa viongozi wa WMO hufanyika kila baada ya miaka minne kwa kuchagua viongozi mbali mbali wakiwemo Katibu Mkuu, Rais, Makamu wa Rais wa kwanza, wapili na watatu, ambapo kwa mwaka huu umefanyika katika mkutano wa 18 wa shirika hilo baada ya muda wa viongozi hao kuisha. Uchaguzi huo ulifanyika kwa haki na kwa mani na kuwapata viongozi hao ambao ni Prof. Petteri Taalas kutoka Finland (Katibu Mkuu), Prof. Dk. Gerhard Adrian kutoka Ujerumani (Rais), Prof. Celeste Saulo kutoka Argentina (Makamu wa kwanza wa Rais), Dr. Albert Martis kutoka Curacao (Makamu wa Pili wa Rais) na Dkt. Agnes Kijazi kutoka Tanzania (makamu wa tatu wa Rais).


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post