Serikali Kufanya Utafiti Na Tathmini Kuhusu Maji Kujaa Kwenye Mashamba

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imearifu kuwa inafanya utafiti na tathmini ya kina ya maji kujaa kwenye mashamba ya wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 10 Juni 2019 wakati akijibu swali la Mhe Yahaya Omary Massare wa Jimbo la Manyoni Magharibi aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani kuwasaidia wananchi kwa kuwajengea mifereji ya kuongoza maji yasiingie mashambani.

Mbunge huyo alisema kuwa Eneo la Mbuga linalozunguka Mji wa Itigi pamoja na kufaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama Mahindi, Alizeti, Choroko na Dengu lakini eneo hili linajaa maji na kufanya kilimo kuwa kigumu.

Mhe Mgumba aliongeza kuwa Utafiti na tathmini hiyo itakapokamilika itakuja na mikakati na mapendekezo stahiki yatakayosaidia kutatua changamoto ya kujaa maji mashambani na kuwasaidia  wakulima wa eneo la mbuga linalozunguka mji wa Itigi ili kuongeza uzalishaji na tija.

Aliongeza kuwa eneo la mbuga linalozunguka mji wa Itigi limekuwa likijaa maji pale mvua zinapokuwa juu ya wastani ambapo historia inaonesha kuwa bonde hili lilijaa maji kipindi cha mwaka 1997/1998 wakati wa mvua za E-lnino na katika msimu wa 2015/2016 baada ya miaka tisa tangu wakati wa mvua za E-lnino mwaka 1997/98.

Aidha, alisema kuwa Serikali imelichukua suala la Mheshimiwa Mbunge na itatuma wataalam wa Kilimo na Tume ya Umwagiliaji kwa ajili ya kwenda kufanya utafiti na tathmini ya kina ya maji kujaa kwenye mashamba ya wakulima.

Utafiti na tathmini hiyo itakapokamilika itakuja na mikakati na mapendekezo stahiki yatakayosaidia kutatua changamoto ya kujaa maji mashambani na kuwasaidia  wakulima wa eneo la mbuga linalozunguka mji wa Itigi ili kuongeza uzalishaji na tija.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments