MKAPA MGENI RASMI UZINDUZI WA MAADHIMISHO YA MIAKA 20 KUELEKEA MIAKA 25 YA CHUO CHA SAUT


Na Eleuteri Mangi- SAUT
Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 kuelekea miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT).

Kwa mujibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu amesema kuwa chuo kimemualika Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika elimu ya juu ambapo uzinduzi wa maadhimisho hayo unatarajiwa kufanyika chuoni hapo Julai, 2 mwaka huu jijini Mwanza.

Akiongea na waandishi wa habari leo chuoni hapo makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof. Mahalu amesema kuwa yapo mafanikio mengi ambayo chuo kinajivunia tangu kuanzishwa kwake mwaka 1998. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 204 hadi wanafunzi 11400 kwa mwaka wa masomo 2018/2019 licha ya kwamba katika mwaka wa masomo 2012/2013 udahili uliwahi kufikia wanafunzi 13121 kabla ya kuongezeka kwa matawi 13 ya chuo hicho.

“Katika mtaala wa chuo, wanafunzi wanapata fursa ya kusoma masomo ya ujasiriamali na kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao na hivyo kuondokana na dhana ya kungoja kuajiriwa. Chuo kimeboresha kiwango cha elimu inayotolewa kuhakikisha wahitimu wanahimili soko la ushindani Afrika Mashariki na duniani kote pia kutokana na elimu ya dini na maadili kwa wanafunzi wote.” Amesema Balozi Prof. Mahalu 


Katika kuunga mkono juhudi za Serikali, Balozi Prof. Mahalu amesema kuwa chuo kimefanikiwa kuanzisha kituo cha kuzalisha na kuwawezesha wajasiriamali ambapo wanafunzi wanaohitimu masomo yao wanapata fursa ya kuandika mawazo ya biashara na baada ya mawazo yao kukubalika hupatiwa mafunzo maalumu juu ya mawazo hayo na kisha wanapatiwa mtaji kati ya shilingi milioni 25 hadi 30 kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.

Aidha, chuo hicho kimefanikiwa kuongeza vitivo vingine vinne (4) kutoka kitivo kimoja ambacho kilikuwa cha Sayansi ya Jamii na Mawasiliano kilichokuwa na shahada moja ya Mawasiliano ya Umma na kuongezeka kwa Kitivo cha Biashara na Utawala, Kitivo cha Ualimu, Kitivo cha Sheria na Kitivo cha Uhandisi.

Zaidi ya hayo Balozi Prof. Mahalu amesema chuo cha SAUT kina mchango mkubwa katika kutoa wanataaluma na wataalam katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wahadhiri, Wanahabari, Wanasheria, Wasimamizi katika taasisi za Fedha na Wakaguzi wa Fedha, Walimu, Wahandisi, Wafanyabiashara, Watunza amani katika majeshi ya Ulinzi na Usalama pamoja na Wanasiasa. Miongoni mwa wahitimu hao ni Mhe. Dotto Biteko Waziri wa Madini, Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, Zawadi Machibya na Sammy Awami ambao ni watangazaji wa BBC, pamoja na wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi ndani na nje ya nchi.

Chuo cha SAUT nje ya taaluma pia kinatoa huduma kwa jamii ambapo kimefanikiwa kuanzisha mradi mkuwa wa umeme wa kutumia nishati ya jua kwa kushirikiana na nchi ya Ujerumani ambapo mradi huo unatekelezwa katika vijiji mbalimbali katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera na Geita. 


Naye Mratibu wa Kamati ya Habari-Maandalizi ya kuelekea miaka 20/25 ya chuo cha SAUT Padre Titus Ngapemba amesema kuwa Rais Mtaafu Benjamin Mkapa amekuwa mdau muhimu katika sekta ya Elimu nchini katika ngazi mbalimbali za uongozi.

Padre Ngapemba amesema kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa amekuwa mdau muhimu katika sekta ya elimu nchini na kwa namna ya pekee katika chuo cha SAUT, akiwa madarakani alifanikisha ujenzi wa barabara ya kutoka jijini Mwanza kuingia chuoni hapo ambapo ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ulianza mwaka 2002 na kuzinduliwa mwaka 2004.”

“Mzee Mkapa anakumbukwa sana kwa kuwa mwasisi wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa vyuo vyote vya umma na binafsi. Uamuzi huu wa Mzee Mkapa wa kuwapatia mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi umesaidia Watanzania wengi kusoma elimu ya juu. Kwa hili utakumbukwa Mzee Mkapa” alisisitiza Padre Ngapemba.

Padre Ngapemba aliendelea kusema “Kwa mara ya kwanza mwaka 2005 Serikali ya Awamu ya Tatu ilibadilisha Sera ya mikopo ya elimu ya juu na kuanza kutoa mikopo kwa vyuo vikuu binafsi ikiwemo SAUT baada Makamu wa Mkuu wa chuo wa wakati huo Padre Deogratius Rweyengeza kutoa ombi hilo wakati wa mahafali ya kwanza mwaka 2001 tangu kipandishwe hadhi.”

Chuo Kikuu cha SAUT kinamilikiwa na kusimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kimeanzishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka 2005 ambapo awali kilikuwa kinajulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii Nyegezi (NSTI) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na wamisionari wa kanisa katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika wakiwa chini ya Askofu Mkuu Joseph Blomjous wa Jimbo Kuu la Mwanza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post