NDUGAI KUWAONGOZA WABUNGE KWENDA MISRI KUSHUHUDIA AFCON


Spika wa Bunge Job Ndugai anatarajiwa kuwaongoza Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushuhudia mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) Nchini Misri.

Mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza June 21 mwaka huu nchini Misri ambapo Tanzania imepangwa Kundi C pamoja na Nchi za Kenya, Algeria na Senegal.

Akizungumza leo Juni 10, bungeni mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Spika Ndugai amesema ataenda kushuhudia fainali hizo.

 “Na wale wa awamu ya kwanza kama siku zile nne ni chache na mimi nitalipia nitaenda na wale wa awamu ya kwanza hivyo  tunaweza kuwa pamoja,”amesema.

Akizungumzia utaratibu wa safari na gharama zake, Spika Ndugai amesema kutakuwa na awamu mbili za safari za kwenda Nchini Misri.

“Awamu ya kwanza ambayo itakuwa ya siku nne gharama zake ni Dola za Marekani 720 ikijumuisha tiketi za kwenda na kurudi, usafiri wa kwenda uwanjani na kurudi hotelini na malazi.

“Mwenyekiti wa Bunge Sc Club, William Ngeleja, anaawatangazia na kuwaombeni kwa ambao tunapenda kushuhudia fainali za AFCON nchini Misri mwaka huu tuendelee kujiandikisha kupitia kwake, Ester Matiko, John Kadutu,Venance Mwamoto, Sixtus Mapunda na Cosato Chumi wale ambao tungependa kwenda.

“utaratibu mzima wa safari umeishatolewa kupitia mitandao yetu ya bunge gharama za safari unachagua mwenyewe kama unataka kwenda awamu mbili ama moja,”amesema Ndugai.

Amesema awamu ya pili ambayo itakuwa ya siku sita gharama zake ni dola za Marekani 770 kwa kichwa.

“Awamu ya pili ni ya siku sita hii gharama zake ni dola 770 tu kwa hiyo ukitaka kukaa siku zote ni sawa tu, ‘Atleast’ awamu mojawapo waheshimiwa Wabunge tunaweza tukashiriki, ”amesema.

Aidha Spika amewaomba Wabunge kwenda kuiunga mkono Taifa Stars ili wachezaji wajione wanadeni kwa taifa.

“Tunaomba sana waheshimiwa Wabunge tuunge mkono sana timu yetu ni miaka mingi sana hatujafika AFCON kwahiyo wachezaji wakiwa wanacheza wanaona wabunge wamekuja kuwaunga mkono naamini itawapa  nguvu kubwa zaidi,”amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527