MBUNGE WA KAHAMA MJINI AISHAURI SERIKALI IFUTE TOZO YA MAITI KWENYE CHUMBA CHA KUHIFADHIA MAITI [MORTUARY]

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

Michango ya Wabunge ya kuchangia maoni mbalimbali  juu ya bajeti kuu ya Serikali imeendelea bungeni jijini Dodoma ambapo mbunge wa Kahama mkoani Shinyanga,Jumanne Kishimba maarufu kwa jina Prof.Kishimba ameitaka serikali kufuta tozo la Maiti kwenye chumba cha kuhifadhia  maiti [Mortuary]

Mhe.Kishimba ameshangaa  kufuta na kusamehe  tozo kwenye unga wa  ngano huku tozo la Maiti kwenye Mortuary ambayo ni Tsh.Laki tano  ikiwa inaendelea hivyo ameishauri serikali kurudisha tozo ya keki na kuweza kufuta tozo ya maiti.

Mhe.Kishimba amesema ni jambo la kushangaza kwa watu wanaofariki kwa waganga wa jadi hawadaiwi bili yoyote  na hupewa huduma ikiwa ni pamoja na sanda lakini mtu anapofariki akiwa hospitalini anadaiwa bili kubwa hivyo ni vyema serikali ikaangalia upya suala hilo kwani hali hiyo husababisha baadhi ya maiti hukosa ndugu wa kuichukua hospitalini kwa kukwepa kulipa bili  na tozo ya Mortuary kutokana  na hali ngumu ya Maisha na kusababisha kuzikwa ovyo.

“Mnajua waheshimiwa wabunge sisi ni  marehemu watarajiwa ,kasoro itakuwa  muda,tarehe na wakati,tumesamehe tozo ya keki lakini kwenye tozo ya maiti inabaki palepale,haiwezekani mtu apoteze mtu halafu atozwe bili na fedha ameitoa wapi”Amesema.

Mbunge Kishimba amesema yawezekana watengeneza Bajeti wanaishi Osterbay hawajui hali ngumu za watanzania kwa kufuta tozo ya keki ambayo kwa watanzania walio wengi amedai haina tija kwao na hivyo kuna haja ya  serikali kurudisha tozo hiyo na kufuta tozo ya Maiti kwenye Mortuary.

Aidha ,Mhe.Kishimba ameiomba serikali iruhusu wananchi pindi wanapoenda kutibiwa ikiwa  hawana fedha waende na mifugo yao hospitalini kama dhamana ili kutibiwa haraka na kuokoa Maisha yao  kwani  bado kuna dhana ya baadhi ya jamii  kanda ya ziwa kutokuwa na uelewa juu ya bima kwani  hudhani kuwa kukata bima ni kujitakia ugonjwa au kifo na elimu inatakiwa itolewe  zaidi.

Sambamba na hayo,Mhe,Kishimba amesema kuna haja kubwa ya serikali kupunguza tozo za X-RAY  ili watu wengi wanunue na kupekeka hospitalini  hali itakayosaidia kupata huduma za X-Ray kwa bei nafuu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post