WAZIRI LUGOLA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KITUO CHA POLISI STAKISHARI DAR

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amefanya ziara ya kushtukiza Kituo cha Polisi Stakishari jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia utendaji kazi wa Kituo hicho.


Waziri Lugola aliwasili kituoni hapo Saa 6:16 mchana ambapo alikutana na wananchi mapokezi ya kituo hicho ambao walifika kwa ajili ya kuwachukulia dhamana ndugu zao walipo katika mahabusu ya kituo hicho, aliwahoji kama wanapata huduma nzuri kutoka kwa askari wa kituo hicho.

Pia Waziri Lugola akiwa katika mapokezi ya kituo hicho, alikichukua kitabu cha taarifa za watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu hiyo akiwahoji watuhumiwa wote kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.

Akizungumza mara baada ya kumaliza kuiwahoji mahabusu hao, alisema ziara yake ni ya kawaida ya kufuatilia utendaji kazi wa vituo vya polisi, pia kufuatilia ahadi zake ambazo alizitoa Bungeni kufuatilia vituo mbalimbali vinavyolalamikiwa, na pia yeye Waziri ni wajibu wake kufuatilia utendaji kazi pamoja na maagizo anayoyatoa mara kwa mara ya dhamana zitolewe saa 24 ikiwemo Jumamosi na Jumapili na pamoja na polisi kutowabambikizia kesi wananchi.

“Lengo la hii ziara yangu ni kuboresha utendaji kazi wa vituo vya polisi nchini, sijaja kumuadhibu mtu mimi, hivyo msiwe na wasiwasi, bali kilichonifanya hapa nije nikufuatilia maagizo mbalimbali ambayo niliyatoa kama kweli mnayafanyia kazi,” alisema Lugola.

Lugola aliwataka Makamanda wa polisi mikoa mbalimbali nchini, kusimamia utendaji kazi bora na kuakikisha maagizo yake anayoyatoa yanafanyiwa kazi ipasavyo, na ataendelea kuyafuatilia maagizo yote anayoyatoa na endapo yakipuuzwa hatamvumilia mtu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527