UJENZI WA BWAWA LA MBAGALA WATAKIWA KUKAMILIKA, WAFUGAJI KUNUFAIKA


Na. Edward Kondela
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameutaka uongozi wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) uliopo chini ya Wizara ya Maji, kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Mbangala lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songwe iliyopo Mkoani Songwe ili kutatua kero za wananchi kukosa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo na pia kuondoa migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.


Prof. Gabriel amebainisha hayo alipotembelea eneo hilo kushuhudia ujenzi wa bwawa ambapo amesema anaridhishwa na ubora na viwango vya ujenzi japo amesisitiza kwamba DDCA waongeze kasi ya kazi hiyo ili iishe mapema iwezekanavyo ili kukidhi mahitaji ya wafugaji kama ilivyokusudiwa. Sambamba na hilo amehimiza uiongozi wa juu wa DDCA kuzingatia maelekezo na ushuri wa kitendaji ambao amewapatria na wawasilishe ripoti ya utekelezaji katika muda walioyoelekezwa.  

Katibu mkuu huyo amesema kulingana na ibara ya 25 ya ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 inaelekeza kuna haja ya kuongeza malambo, mabwawa na visima virefu katika maeneo yanayohitaji maji na malisho.

“Lengo la wizara ni kuhakikisha tunaondokana na kadhia ya maeneo ya malisho na maji kwa mifugo katika maeneo yote nchini ili kuhakikisha sekta ya mifugo inaimarika.” Alifafanua Prof. Gabriel

Kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumaji wengine wa ardhi Katibu Mkuu huyo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha migogoro inaondoka katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa.

Kwa upande wake Msaidizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Bw. Evance Kulanga amesema Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ina idadi kubwa ya ng’ombe wapatao 680,000 ikiwa ni idadi kubwa ya ng’ombe kuliko wilaya zote zilizopo Mkoani Songwe, hivyo kutoa rai kwa wananchi kulitunza bwawa hilo mara litakapokamilika.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbangala linapojengwa bwawa la kunyweshea mifugo Bw. Revocatus Nkonoki amesema bwawa litanufaisha wafugaji  kwa kuwa kata hiyo ina ng’ombe Elfu Nne na wafugaji katika kata hiyo wamekuwa wakiuliza mara kwa mara juu ya kukamilika kwa bwawa hilo ili waweze kupata maji kwa ajili ya mifugo yao.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi wa Mabwawa katika Idara ya Mabwawa katika Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) uliopo chini ya Wizara ya Maji Mhandisi Sadara Sadick amesema atayafikisha maagizo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulika Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ili waweze kukamilisha ujenzi wa bwawa mwaka huu.

Bw. Sadick amesema watafika katika ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tarehe 24 mwezi huu kama walivyoelekezwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ili waweze kujadiliana na wizara juu ya utekelezaji wa haraka wa mradi huo.

Ujenzi wa bwawa la maji la Mbangala kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo umeanza kutekelezwa rasmi mwezi Novemba Mwaka 2018 ambapo mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu Shiling Bilioni Moja.

Imetolewa: Kitengo cha Mawasiliano Serikalin                   Wizara ya Mifugo na Uvuvi


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post