TAASISI ZA DINI ZINAZOANZISHA HOSPITALI ZATAKIWA KUWEKA GHARAMA NAFUU KWA WANANCHI


Rais  John Magufuli amezitaka taasisi za dini zinazoanzisha hospitali kuweka gharama nafuu kwa wananchi ili waweze kumudu kupata huduma za matibabu,kutobagua dini, madhehebu wala kabila.

 Rais ameyasema hayo jana wakati akifungua hospitali ya Uwata (Umoja wa Uamsho wa Wakristo Tanzania) iliyopo jijini Mbeya yenye uwezo wa kulaza hadi wagonjwa 134 kwa siku.

“Pia endapo mgonjwa asiye na uwezo wa kumudu gharama za matibabu amefika katika hospitali hizo hawatakiwi kumfukuzwa kwa sababu inawezekana ni malaika amefika kuwajaribu katika utoaji huduma,” alisema kwa utani.

Rais Magufuli alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuchangia uendeshaji wa hospitali binafsi ili kuhakikisha huduma zinazotolewa gharama yake inakuwa nafuu na kila mtu anaweza kumudu.

“Sisi Watanzania siyo wote wenye uwezo wa kulipa gharama kubwa, upo mchango wa Serikali ikiwamo katika ulipaji wa mishahara, hata mashuka niliyoyakuta mle hata vifaa vingine inawezekana vimetolewa na Serikali kwahiyo Uwata inakuwa msimamizi ikishirikiana na Serikali hivyo gharama isije ikawa kubwa sana ikawaumiza wananchi hawa.

“Hospitali hizi zinahesabika kama zinatoa huduma kwa watu, kuwa ni mahali ambapo watu wanapakimbilia kwenda kutibiwa na kupata uponyaji, ninyi mnasimama badala ya Mungu, ninyi mnasimama badala ya Yesu ambaye alikuwa akiwaponya wanasimama na kurudi nyumbani bila kudai hela,” alisema.

Aidha, Rais Magufuli ameahidi kujenga barabara ya lami kutoka Mabanzini hadi katika eneo la hospitali hiyo yenye urefu wa mita 700.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post