Bodi ya Ligi Kuu (TPLB): STAND UNITED IMESHUKA DARAJA...KAGERA SUGAR IMEBAKI

Utata uliojitokeza wa timu ipi itaungana na African Lyon kushuka daraja baada ya msimu kumalizika, umehitimishwa rasmi leo baada ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kutangaza rasmi kuwa Stand United ya Shinyanga imetereka daraja baada ya kumaliza nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi.

Sintofahamu hiyo iliibuka baada ya msimamo wa mwisho wa ligi uliotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuonyesha kuwa Kagera Sugar ndio inapaswa kushuka daraja ikizidiwa idadi ya mabao ya kufunga na Stand United.

Msimamo huo ulionyesha kuwa timu hizo zote zina idadi sawa ya pointi ambazo ni 44, huku kigezo cha pili cha kuamua mshindi baina yao ambacho ni kutazama utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa pia wakiwa sawa kwa maana ya timu zote mbili kuwa na mabao -11.

Kwa mujibu wa msimamo huo uliotolewa na TFF, Stand iliwekwa juu ya Kagera Sugar kwa kutazama kigezo cha tatu ambacho ni uwingi wa mabao ya kufunga ambapo wao walikuwa na mabao 38 huku Kagera wakiwa nayo 33.

Hata hivyo msimamo huo wa ligi uliotolewa na TFF ulionekana kuwa na makosa kwani kwa mujibu wa matokeo halisi ya timu hizo, Kagera walimaliza wakiwa na utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa -10 huku Stand United wakiwa na -12 na ndio walipaswa kushuka.

Akizungumza jijini leo, Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura alisema baada ya bodi na TFF kupitia upya takwimu za ligi, Stand United ndio timu itakayoshuka daraja.

Na Charles Abel - Mwanaspoti

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527