SIMBA SC YATWAA TENA UBINGWA WA LIGI KUU YA BARA


Simba SC wamefanikiwa kutetea taji lao ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Singida United jioni ya leo Uwanja wa Namfua.

Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems imefikisha pointi 91 baada ya ushindi wa leo katika mchezo wa 36 ikijihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu, kwani hakuna timu inayoweza tena kuwafikia. 

Hilo linkuwa taji la pili mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu kwa Simba SC na la 19 jumla kihistoria baada ya awali kulibeba katika miaka ya 1972, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007, 2010, 2012 na 2018.

Watani wao, Yanga SC ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa Ligi Kuu, mara 26 wakiwa wamebeba taji hilo miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.

Timu nyingine zilizowahi kubeba taji hilo ni Cosmopolitan 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar mara mbili 1999 na 2000 na Azam FC 2014.

Katika mchezo wa leo, mabao ya SImba SC yalifungwa washambuliaji wake tegemeo, Meddie Kagere kutoka Rwanda kipindi cha kwanza na mzawa, John Raphael Bocco kipindi cha pili.

Kagere alifunga bao lake dakika ya tisa tu akitumia makosa ya beki Kennedy Wilson Juma kuzubaa na mpira kufuatia krosi ya beki wa kushoto wa Simba SC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye pia ni Nahodha Msaidizi wa klabu. 

Nahodha John Bocco akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 60 akimalizia krosi ya mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyenzishwia mpira wa kurushwa na Tshabalala. 

Hata hivyo, bao hilo kidogo lilikuwa la utata, kwani kwani refa Shomary Lawi kutoka Kigoma aliwaruhusu Simba kuanza mpira wakati kipa wa Singida United, Said Saleh Lubawa akiwa nje anaugulia maumivu baada ya kuumia wakati akiokoa.

Wachezaji wa Singida United walibishana na refa kwa dakika mbili kabla ya mchezo kuendelea, huku kipa Lubawa akibebwa mabegani kutolewa nje nafasi yake ikichukuliwa na David Kissu.

Kikosi cha Singida United kilikuwa; Said Lubawa/David Kissu dk66, Frank Mkumbo, Gilbert Mwale, Salum Kipaga, Kennedy Wilson, Rajab Zahir, Boniface Maganga/Mathew Michael dk78, Issa Makamba, Jonathan Daka, Habib Kyombo na Geoffrey Mwashiuya/Assad Juma dk58.

Simba SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Muzamil Yassin, Haruna Niyonzima/Hassan Dilunga dk79, John Bocco, Meddie Kagere/Clatous Chama dk85 na Emmanuel Okwi/Jonas Mkude dk75.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post