SERIKALI YAIPA AZAM TV LESENI YA KUONYESHA CHANELI ZA NDANI BURE


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amelieleza Bunge leo Jumanne Mei 14, 2019 kuwa kituo cha televisheni cha Azam jana Jumatatu kimepokea leseni ya kuonyesha chaneli za ndani bure na kwamba kampuni hiyo imeahidi kufunga mitambo yake nchi nzima kwa ajili ya kurusha matangazo hayo ndani ya kipindi cha miezi saba.

Nditiye ametoa kauli hiyo akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, aliyehoji ni kwa nini Azam wananyimwa haki ya kuonyesha channel za ndani bure.

"Je, Serikali haioni kuwanyima haki hiyo wakati wengine wamepewa ni kukiuka ibara ya 18 ya katiba ambayo inatoa haki ya kupata habari, lakini hata Rais wetu anatumia Azam kurusha matangazo yake hivyo tungejitangaza hadi nje," ameuliza Shangazi.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula, aliuliza Serikali iwapo haioni kupitia  TCRA kuwafungia local channels (chanel za ndani)  baadhi ya ving'amuzi ikiwamo Azam TV, DSTV na vingine imewanyima wananchi fursa ya kupata habari.

Naibu waziri amesema Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kujua mambo yanayoendelea, hivyo imetoa leseni zenye masharti tofauti.

Amesema kwa sasa matangazo ya umma yanarushwa na TBC1 na TBC3 maarufu safari channel.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post