SERIKALI YA POLAND YAONYESHA NIA YA KUISAIDIA SEKTA YA AFYA NCHINI

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameishukuru Serikali ya Poland kwa kuonyesha nia ya dhati ya kuisadia Tanzania katika Sekta ya Afya Nchini ili kuboresha na kupunguza changamoto katika Sekta hiyo.

Mhe. Jafo ameyasema hayo wakati wa kikao na wadau wa maendeleo katika Sekta ya Afya kutoka Poland cha kujadili masuala mbalimbali yanayouhusiana na Afya na jinsi Nchi hiyo inavyoweza kusaidia kuimarisha na kuboresha Sekta ya Afya nchini.

Mhe. Jafo ameishukuru Serikali ya Poland kwa ushirikiano wanatoa katika Miradi mbalimbali ya maendeleo na kutambua umuhimu wa sekta ya afya nchini kwa kuwa bila kuimarisha Sekta ya afya hakutakuwa na maendeleo na kushindwa kufikia uchumi wa kati.

“Sekta ya afya ni muhimu kwa jamii, jamii isipokuwa na afya bora hakutakuwa na maendeleo, hivyo ni vyema Serikali ikajikita kuwekeza katika Sekta ya afya kwa kuhakikisha inajenga miundombinu bora, uwepo wa vifaa na vifaa tiba ili kuboresha huduma za afya nchini” Amesema Mhe. Jafo

Amesema kuwa hatuwezi kufikia uchumi wa kati endapo watu wetu hawatakuwa na afya bora, ili watu wafanyekazi kwa bidi waweze kuzalisha na kulipa kodi inavyotakiwa wanatakiwa kuwa na afya bora hivyo tunawakaribisha wadau mbalimbali wa Sekta ya afya kuwekeza katika Sekta hiyo.

Mhe. Jafo amendelea kuishukuru Serikali ya Poland kwa kuonyesha nia ya kuisaidia Serikali mkopo wenye gharama nafuu utakaosaidia kuimarisha na kuboresha sekta ya Afya nchini lengo likiwa ni kupunguza changamoto mbalimbali katika sekta hiyo.

Ameiomba Serikali ya Poland kujikita zaidi katika kusaidia kwenye kuimarisha huduma za msingi hasa ujenzi wa Vituo vya afya na upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba kwa kuwa ndipo kwenye changamoto kubwa katika suala zima la utoaji wa huduma na itasaidia kupunguza vifo kwa jamii
Mhe. Jafo amefafanua kuwa katika eneo la Sekta ya Afya Serikali itapata fursa ya kusaidiwa ujenzi wa Vituo vya afya, ambavyo vitakuwa vya mfano kwa kuwa na vifaa vyake na kuwa na nyumba zaidi ya nne za madaktari na hivyo kupunguza changamoto zilizopo.

Mhe. Jafo amelishukuru shirika la Light For Africa kwa kuunganisha nchi ya Poland na Tanzania ambao wameonyesha nia ya dhati katika kusaidia masuala ya Sekta ya Afya nchini jambo ambalo litasaidia kuleta maendeleo kwa jamii

Aidha Wadau hao watatembelea, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hospitali ya Mirembe, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Amana na Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kwa lengo la kuangalia ni namna Tanzania inavyotoa huduma za afya na kuangalia maeneo ambayo wanaweza kusaidia katika kutumia fursa walizonazo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527