JE UMEWAHI KUSIKIA HABARI ZA MWANAMALUNDI?? YULE MSUKUMA MWENYE MIUJIZA?? ....SOMA HAPA


Mwanamalundi ni jina ambalo lilikuwa maarufu sana karne ya 18 na 19 (enzi za mkoloni) maeneo ya kanda ya ziwa; hususani Mwanza na Shinyanga. Habari za huyu mtu zimewahi kuandikwa kwenye kitabu kiitwacho "MWANAMALUNDI: Mtu maarufu katika Historia ya Usukuma". Ni kitabu ambacho kiliingizwa kwenye mtaala wa elimu ya msingi miaka ya 1970-80. Wazee wenzangu watakuwa wanakumbuka. Hivi sasa habari za mtu huyu ni Kama vile zimepotea kabisa.

MWANAMALUNDI NI NANI HASA?

Mwanamalundi ni jina la mtu wa miujiza kutoka kabila la Wasukuma. Matamshi sahihi ya jina hili Ni "Ng'wanamalundi" na sio "Mwanamalundi" kama ambavyo wengi hutamka.

Mwanamalundi alizaliwa kijiji cha Ng'wakwibilinga, wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mwaka 1892. Baba yake aliitwa Bugomola na mama yake aliitwa Ngolo. 

Wazazi hawa wawili hawakujaaliwa kupata watoto kwa muda mrefu sana. Uzee uliwakaribia bila hata kupata mtoto. Jambo hili liliwakosesha sana raha, hasa Mzee Bugomola ambaYe alitamani sana japo apate mrithi wa mali zake. Hali hii ilimfanya Bugomola kuwa mtulivu na mpole muda mwingi katika maisha yake.

Katika jamii ya wasukuma wakati huo, mwanamke asiposhika mimba ndani ya kipindi cha miezi 6 hadi 12 tangu aolewe, ilikuwa ni lazima aende kwa mganga kujua kinachomsumbua.

 Ni nyakati ambazo hakukuwa na makanisa ya maombezi kama ilivyo leo hii, misikiti ya kuomba dua wala hospitali. Waganga ndio watu pekee waliotatua matatizo mbalimbali ya jamii zao.

Mzee Bugomola na mke wake Ngolo wakaamua kwenda kwa mganga upande wa mashariki ya kijiji walichokuwa wakiishi (Ng'wakwibilinga) ili wapate ufumbuzi wa tatizo lao. 

Mganga aliwaambia ujio wao hata kabla hawajajieleza wenyewe. Mganga akawatengenezea dawa kisha akawaambia kuwa Ngolo (mama/mke) atashika mimba na atazaa mtoto wa kiume ambaye atakuja kuwa mashuhuri siku za hapo baadaye lakini kwa bahati mbaya Bugomola (baba/mume) hatoweza kumuona mtoto huyo; yaani Bugomola atafariki kabla mtoto hajazaliwa.

Habari hii ilimfurahisha sana Bugomola pamoja na kwamba aliambiwa atakufa bila kumuona mtoto. Mkewe pia alifurahi kusikia kuwa atashika mimba. Bugomola hakujali kifo chake sababu hata umri wake ulikuwa umeenda kidogo. 

Furaha yake kubwa ilikuwa ni kumpata mrithi wake. Walirudi nyumbani wakiwa na furaha kubwa. Bugomola hakuweza kuificha furaha yake. Muda mwingi alionekana ni mwenye tabasamu na vicheko vingi tofauti kabisa na vile watu walivyozoea kumuona.

Baada ya wiki kadhaa Ngolo alishika mimba. Mimba ilipotimiza miezi mitatu tu, Bwana Bugomola aliaga dunia bila hata kuugua. Ngolo ambae alikuwa mjane wakati huo aliilea mimba hiyo hadi ilipofikisha miezi 9.

Siku moja kabla Ngolo hajajifungua mtoto, wingu kubwa lilitanda angani. Mvua kubwa na yenye radi kali ikaanza kunyesha. Mtoto aliyekuwa tumboni akaruka mruko usio wa kawaida na kisha ikaskika sauti ya kitoto kutoka tumboni ikisema, "Mayu nibyalage, yaani mama nizae!"

 Ngolo akashtuka na kuingiwa hofu baada ya kusikia sauti hiyo, hivyo akamuita mama mkwe wake na baadhi ya majirani ili nao waweze kuwa mashahidi wa sauti hiyo. 

Kwa bahati nzuri sauti ile ikajirudia tena na ghafla uchungu ukamshika Ngolo. Ilikuwa ni mwaka 1892 Ngolo alipojifungua mtoto wa kiume mwenye maajabu tangu akiwa tumboni mwake. Mtoto huyo akaitwa Igulu, yaani Mbingu.

Igulu (Mwanamalundi) alizaliwa akiwa mwenye afya njema kabisa isipokuwa tu miguu yake ilikuwa myembamba na yenye nyayo kubwa tangu alipozaliwa. Kutokana na wembamba wa miguu yake, jamii ikampa jina la utani "Mamilundi" likimaanisha "mamiguu membamba".

Igulu alikuwa ni mtu mwenye aibu sana enzi za utoto wake. Alikuwa akiwakimbia wageni wasimuone na kuuficha uso wake kwa aibu. Pamoja na aibu alizokuwepo nazo, alipenda sana kuzurura mitaani akiwa ameambatana na marafiki zake.

 Baadhi ya wazazi hawakupendezwa na tabia yake ya uzururaji akiwa ameambatana na watoto wao. Mara kadhaa wazazi wa marafiki wa Igulu walimtamkia Igulu (Mwanamalundi) maneno mabaya kila Igulu (Mwanamalundi) alipotoka kuzurura na watoto wa majirani zake, walimwambia, “Mamilundi galyo lilihumbura bana bise”, ikiwa na maana "mamiguu yake marefu linarubuni watoto wetu”.

Katika ujana wake Igulu, alipenda sana kucheza ngoma aina ya Kahela. Kila aliposhiriki kucheza ngoma hiyo, alipenda sana kuuficha uso wake kwa kitambaa cheusi. Katika mashindano ya kucheza ngoma hiyo, Igulu na marafiki zake walishindwa kuwa washindi. 

Watu kama Samíke, Ng'wanikinga, Ng'wanilong'ho na Gíndù Nkíma walikuwa si rahisi kuwashinda katika uchezaji wa ngoma. Ni watu ambao walijua kucheza ngoma kwa umahili kuliko Igulu (Mwanamalundi). Mara nyingi matumizi ya uchawi yalihusika katika kuwapa ushindi wa kucheza ngoma hiyo na kukubalika kwa watu mbalimbali.

Kutokukubalika kwa Igulu (Mwanamalundi) na marafiki zake mbele ya jamii hasa katika uchezaji wa ngoma kulipelekea achukue uamuzi wa kwenda kwa mganga. Igulu aliwashawishi vijana wenzie waende kwa mganga atakayewapa dawa ya mvuto kwa watu na kuwa washindi nyakati zote za mashindano ya ngoma. Vijana wenzie walikubali sababu kwa nyakati zile suala la kwenda kwa mganga lilikuwa ni jambo dogo sana.

Safari ya kuelekea mashariki zaidi mwa kijiji chao ikawadia. Mganga alikuwa ni mwanamke, mwenye umri ufaao kuitwa bibi ndani ya kijiji cha Nyaraja, wilaya ya Iramba mkoa wa Singida. Walipokelewa vizuri na mwenyeji wao. Iliwachukua wiki moja bila kuhudumiwa chochote kile, siku ya nane mganga akawaamuru wachukue panga na majembe kuelekea porini ili wakachimbe dawa itakayowasaidia kupendwa na watu.

Wakiwa porini, yule bibi mganga alitafuta vinyonga watatu kwa idadi ya vijana hao wanaotaka dawa kisha akawaambia wachimbe mashimo yenye nusu ya urefu wao. Vijana wakachimba mashimo hayo huku wakiwa na vinyonga vichwani mwao. Walipomaliza kuchimba, bibi mganga akawaambia wafunike mashimo hayo kwa kuni kavu. 

Vijana hao wakatii maagizo ya bibi mganga na kisha bibi akawatoa vinyonga waliokuwa wameng'ang'ania kwenye vichwa vya vijana hao watatu na kisha akawatia dawa midomoni vinyonga hao na kisha akawaweka juu ya kuni zilizofunika mashimo yale yaliyochimbwa na vijana wale watatu. Mara baada ya kuwaweka vinyonga hao juu ya kuni zile, moto ukawashwa ili kuwachoma vinyonga hao.

Hazikupita dakika kadhaa wakiwa wanashuhudia kuteketea kwa vinyonga hao, ghafla akatokea kifaru katika mazingira ya kutatanisha na akaanza kuwafukuza watu wote, akiwemo yule bibi mganga. Igulu (Mwanamalundi) ilimlazimu apande juu ya mti kujinusuru na madhira hayo. Wale vijana wawili walitimka mbio na hawakurudi tena.

 Bibi mganga akararuliwa na yule kifaru mpaka akapoteza maisha na kisha kifaru akamjia Igulu (Mwanamalundi) aliyekuwa juu ya mti na kuanza kuudhuru ule mti kwa pembe yake. Kifaru hakufanikiwa kuuangusha mti aliopanda Igulu zaidi ya kuubandua magome yake. Kifaru alipochoka akaamua kuondoka na kutokomea kusikojulikana.

Igulu (Mwanamalundi) akashuka juu ya ule mti na kumwendea bibi mganga ambaye muda huo alikuwa ni marehemu. Igulu akaubeba mwili wa yule bibi mganga na kuurudisha nyumbani.

 Akiwa njiani, ule mwili wa bibi mganga uliokuwa mabegani mwake ukaonesha kuwa ni kama vile unavuta pumzi mapafuni. Ghafla yule bibi akapiga chafya na kuamka kisha akamuuliza Igulu (Mwanamalundi), "Bhaja hálí abhayanda abhalaha" akimaanisha kuwa wako wapi vijana waliokuwa hapa? Igulu akamwambia kuwa wale vijana wenzie wamekimbia baada ya kumuona yule kifaru. 

Bibi mganga ambaye muda huu alionekana kuwa ni mzima kabisa na hana majeraha tena akaomba warudi eneo la tukio ili wachukue dawa. Wakiwa njiani kurudi eneo la tukio, yule bibi mganga akamsifia sana Igulu kwa kumuita "Ni mwanaume kamili" aliyekuja kweli kutafuta dawa.

 Bibi akaokota yale magome yaliyobanduliwa na kifaru na kisha kuondoka nayo.

Walipofika nyumbani, yule bibi akaamua kumwambia ukweli Igulu (Mwanamalundi) kuwa yule kifaru ni yeye mwenyewe bibi. Aliamua kujibadili ili kuwapima uwezo wao wa kuvumilia magumu. Kwa kuwa Igulu pekee ndio alionesha yuko imara, bibi yule alimtunuku dawa nzuri zitakazompa mvuto na nguvu katika ngoma zake. 

Wale vijana wawili walipitiliza hadi kwao bila kurudi tena kwa mganga. Bibi mganga alimpa masharti Igulu baada ya kumpa dawa. Bibi mganga alimzuia Igulu (Mwanamalundi) kumparaza mtu yeyote au kumnyooshea kidole. Iwapo atafanya hivyo basi alieparazwa au kunyooshewa kidole atakufa hapohapo.

Igulu (Mwanamalundi) aliporudi kijijini kwake na kisha kucheza ngoma ya kwanza baada tu ya kurudi kutoka kwa mganga, alishinda. 

Kuna nyakati Igulu aliamua kucheza ngoma akiwa juu ya jiwe kubwa. Wakati akicheza ngoma hizo, nyazo zake zilionekana juu ya mawe aliyokuwa akitumia kucheza ngoma.

 Ni alama za nyayo ambazo zipo mpaka leo pale kijiji cha Nyandekwa, wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga. Ni kama km 10 tu kutoka makao makuu ya wilaya. 

Kuna nyakati Igulu alitengeneza mashimo ya mchezo wa bao juu ya jiwe kwa kutumia kisigino chake. Ni alama ambazo pia bado zipo kijiji cha Nyandekwa, Kahama-Shinyanga.

Igulu aliposhinda mashindano ya ndani ya kijiji, akaamua kuomba kushindana na wapinzani wakubwa zaidi walioishi kijiji cha Ng'wagala wilaya ya Maswa; yaani akina Samíke, Ng'wanikînga, Ng'wanilog'ho na mwanamke mwenye nguvu za kiganga aitwae Gíndü Nkíma. Hawa watu wanne walikuwa hawana mpinzani katika ngoma lakini Igulu (Mwanamalundi) akajitosa kushindana nao kwa mara nyingine.

Mwanamalundi alipofika kwenye mashindano, akafanya miujiza kwa kujirefusha kama ngongoti asiye na magongo yoyote yale na kisha akaanza kucheza huku akiwa ameficha uso wake kwa kitambaa cheusi kama kawaida yake.

 Wakati anacheza ngoma akiwa ana urefu wa ngongoti, baadhi ya watu walijaribu kugusa na kuifunua miguu yake ili wajue kulikuwa kuna nini. Wote waliothubutu kuigusa walikufa baada ya muda mfupi. 

Katika ngoma hiyo, Gíndü Nkíma akatumia nguvu zake za kiganga kumrudisha Igulu (Mwanamalundi) kama alivyokuwa awali; yaani pasipo kurefuka kama ngongoti. Kwa kufanya hivyo, Mwanamalundi alipoteza pambano hilo.

Mwanamalundi akaondoka Maswa na kwenda kijiji cha Nela ambako lilipangwa shindano jingine. Shindano hili Mwanamalundi alishinda.

 Kwa kuwa katika safari zake zote huambatana na jopo la wapishi wa chakula, ushindi huu ulimkwaza Gíndü Nkíma, mpinzani wake mkubwa ambaye aliamua kuloga chakula anachoandaliwa Mwanamalundi ili kisiive hata kikipikwa wiki nzima.

Ni kweli kabisa, wapishi wa Mwanamalundi walilalamika kuhusu chakula kutoiva kabisa kwa muda mrefu na kuni zinakaribia kuisha. Hivyo wapishi wakaomba msaada wa kuni kwa Mwanamalundi. Baada ya wapishi kulalamika, Mwanamalundi akasonta/akanyoosha kidole kwenye pori fulani eneo hilo na kuwaambia wapishi waende wakakate kuni alikonyooshea kidole. 

Kwa bahati mbaya wakati ananyoosha kidole hicho hakujua kama ndani ya pori hilo kulikuwa kuna mifugo na wachungaji kadhaa ambao wote walikufa na kukauka kama kuni.

Tukio hili la kukausha miti na kuua ng'ombe na wachungaji wake lilimuudhi sana Mtemi Masanja wa III ambaye aliamuru askari wake waende kumkamata Mwanamalundi haraka iwezekanavyo ili awajibishwe.

 Askari wa Mtemi Masanja waliogopa sana kumkamata Mwanamalundi wakihofia kufa. Iliwalazimu kumkamata tu sababu walimuogopa zaidi mtemi kuliko Mwanamalundi.

Kabla Mwanamalundi hajakamatwa, alijua jambo hilo lingetokea. Hivyo akaenda haraka kumuaga mama yake mzazi na kumuachia maagizo. 

Mwanamalundi alikamua maziwa kiasi fulani kwenye kikombe na kisha akampa mama yake na kumwambia, "Iwapo maziwa haya yataanza kuganda, ujue kuwa nipo katika hali mbaya, iwapo yataganda kabisa, ujue kuwa nimekufa!"

 Mwanamalundi akachukua shoka isiyo na mpini kisha akaiegamisha ukutani na kumwambia mama yake, "Iwapo nitakamatwa na kupelekwa kuuliwa, shoka hii itakuwa ikipanda ukutani nikiwa napelekwa kuuliwa, tukifika eneo nitakalouliwa, basi hii shoka itapandisha hadi mwisho wa ukuta kuonesha kuwa tumefika mwisho wa safari!" Mama yake alipokea maagizo hayo na haikuchukua muda Mwanamalundi akakamatwa na askari wa Mtemi Masanja.

Mtemi Masanja III aliamua kupeleka shauri hilo kwa watawala wa kizungu (Wajerumani) ili wamchukulie hatua Mwanamalundi.

 Uchunguzi ukafanyika na Mwanamalundi akaonekana ana hatia ya mauaji ya watu wasio na hatia. Adhabu ya kosa hili ilikuwa ni kunyongwa.

Katika safari hii ya kunyongwa, Mwanamalundi aliambatana na Makongoro Igana ambaye alikuwa ni Mtemi wa Ilemela.

 Mtemi huyu alikuwa ana hatia ya kuwachapa fimbo wajerumani baada ya kupita upande usio sahihi katika njia kadiri ya utaratibu wa utawala wake. 

Mtemi Makongoro Igana kila alipokuwa akisafiri juu ya punda, mkono wake wa kuume ulikuwa umeshika fimbo ndefu. Fimbo hiyo hutumika kumchapia kila atakaepita upande wa kuume katika safari zake. Kwa bahati mbaya wajerumani hawakujua utaratibu huo wa Mtemi Makongoro.

 Siku wajerumani walipopishana safarini na Mtemi Makongoro, walipita upande wa kuume wenye fimbo. Mtemi Makongoro akawachapa fimbo wazungu hao kama ilivyo jadi yake. Wazungu hao walishindwa kumvumilia, wakamkamata na kumfungulia mashtaka yaliyoamuru Mtemi anyongwe.

Kaliyaya ni mtu wa pili aliyeambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa. Huyu Kaliyaya alikuwa ni mtu aliyeonekana ni mwenye ushawishi mkubwa kwa watu wa jamii yake. Kukubalika kwake kulimfanya apate wafuasi wengi ambao walihofiwa kumpindua mjerumani. 

Hivyo wajerumani wakaona ni bora wamfungulie mashtaka ili wamnyonge kabla hajawapindua. Kaliyaya alikuwa ni mtu wa kawaida tu ila ni mwenye ushawishi na kipenzi cha watu wengi.

Mtu wa tatu aliyeambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa ni Mtemi Italange wa Bugando. Mtemi huyu aliingia mgogoro na Wajerumani baada ya kuhodhi eneo kubwa la pwani ya ziwa Victoria na bandari zake kisha akakataa kuwapa Wajerumani. Ili kumnyang'anya utajiri huo, wajerumani wakaamua kumfungulia mashtaka ili wamnyonge.

Zoezi la kunyongwa lilipofika, Mwanamalundi alikuwa ndio mtu wa kwanza kuvishwa kitanzi. Kamba ilipofyatuliwa tu ili kumuua, kamba ikakatika yenyewe. Zoezi la kumuua likaahirishwa, badala ya kunyongwa akabadilishiwa adhabu.

Ikaja zamu ya Mtemi Makongoro Igana. Mtemi alipowekewa tu kitanzi shingoni na kisha kuifyatua kamba hiyo ili kumuua, ghafla kukatokea mfano wa sinema kwenye ukuta. Ni sinema ya kimiujiza iliyoonesha matukio ya kivita miaka ya nyuma.

 Askari wakageuka kuitazama sinema hiyo. Sinema haikuchukua zaidi ya dakika moja, ikaisha. Walipomgeukia yeye (Mtemi Makongoro Igana) wakaona hana kamba shingoni. Huyu naye akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu.

Akaja Mtemi Italange. Huyu alipowekewa kitanzi shingoni, nae pia kamba ilifyatuka. Akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu. Ilipofika zamu ya Bwana Kaliyaya, kitanzi kilipofyatuliwa ili kumnyonga, hakika kitanzi kilimuua. Huyu hakuwa mwenye ulinzi wowote ule kishirikina; yaani alikuwa ni mtu wa kawaida tu.

Ndipo mamlaka za mjerumani zikaamuru askari wawapeleke watu hao watatu Tabora. Wakiwa njiani kuelekea Tabora, walifika Nzega na kuamua kupumzika kidogo chini ya mti mkubwa nje ya Shule ya Sekondari Chama.

 Askari wakijerumani wakawa wakimuuliza maswali Mwanamalundi kuhusu nguvu zake na kisha wakamuomba afanye muujiza wa mwisho kabla hajafikishwa gerezani.

 Mwanamalundi akawaambia askari kuwa bado ana uwezo mkubwa, hata huo mti waliopumzikia anaweza kuukausha.

 Aliongea maneno hayo huku akiupigapiga mti huo. Kabla hajamalizia sentensi yake kuwa anaweza kuukausha, mti ulikauka palepale na majani makavu yakaanza kudondoka. Askari wa kijerumani waliogopa sana tukio hilo.

Walipofika Tabora mjini, Mwanamalundi na wale watemi wawili waliunganishwa na watu wengine wenye makosa ya uhaini na uhujumu uchumi na kisha kupelekwa kisiwa cha Mafia kutumikia kifungo cha miaka mitatu.

Akiwa gerezani, Mwanamalundi aliwekwa chumba kimoja na mtemi Makongoro Igana. Mtemi Makongoro akamuuliza Mwanamalundi, "Hivi huna namna ya kujiokoa mahali hapa?" Mwanamalundi akamjibu kuwa kwa wakati huo hangeweza kujiokoa, ila kuna miujiza ya shoka na maziwa amemuachia mama yake nyumbani. Mtemi akamuuliza, "Una miujiza mingine yoyote?" Mwanamalundi akamwambia Mtemi Makongoro kuwa yeye (Mwanamalundi) anaweza kupanda viazi na mihogo na ikavunwa ndani ya dakika kadhaa tu na ikawa tayari kabisa kwa chakula.

 Wakiwa kisiwani hapo, wakakubaliana kwenda ng'ambo ya kisiwa (bara) kisha wakachukue mbegu za viazi na mihogo ili washuhudie miujiza hiyo ya kupanda na kuvuna ndani ya dakika kadhaa.

Kwa kuwa nyakati hizo wafungwa wa visiwani walikuwa wakiachwa huru sababu hawataweza kutoroka, Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walienda mpaka baharini ndani ya kisiwa hicho.

 Makongoro akiwa ameshika jiwe na Mwanamalundi akiwa ameshika fimbo. Makongoro aliporusha jiwe umbali mrefu baharini, Mwanamalundi aliyapiga maji kwa fimbo na kisha maji yakajitenga na kuacha njia mpaka pale lilipotua jiwe. Walifanya hivyo mpaka walivyofika bara (mainland). Wakatafuta mbegu za mihogo na viazi na kuonesheana miujiza.

Kila walipokuwa wakitoroka gerezani, waliacha vivuli vyao vilivyoonekana kama watu halisi. Kuna nyakati Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walionekana wakiwa Mwanza au Shinyanga na gerezani pia muda huo huo. Jambo hili liliwachanganya sana wajerumani.

Walipomaliza kifungo chao walirudishwa nyumbani kwao kwa ndege. Jamii ya Mwanamalundi ilipoona ndugu yao amerudishwa kwa ndege wakaamua kumpa jina jipya, "Ng'wenhwa ndege", wakimaanisha "aliyerudishwa kwa ndege". Mwanamalundi anaaminika kuwa ndiye msukuma wa kwanza kupanda ndege.

Wakati anarudishwa nyumbani baada ya kumaliza kifungo chake, mama yake alifurahi sana. Mama yake alifurahi kwa sababu maziwa hayakuganda kwa miaka mitatu jambo ambalo lilionesha kuwa huko aliko alikuwa hai. 

Maziwa yalibaki katika ubora uleule kwa miaka mitatu. Shoka ilianza kuteremka taratibu kwenye ukuta kadiri Mwanamalundi alivyokuwa akikaribia kufika nyumbani. Alivyofika tu, shoka ilikuwa tayari imefika ardhini kuashiri kuwa muda wowote Mwanamalundi atafika hapo. Na ndivyo ilivyokuwa.

Aliporudi mtaani, Mwanamalundi hakuacha asili yake. Aliendelea kucheza ngoma maeneo mbalimbali. Mtemi Masanja ambaye ndiye aliesababisha Mwanamalundi kunusurika kunyongwa na hatimae kufungwa, aliamua kumfukuza Mwanamalundi katika himaya ya utawala wake.

 Mwanamaundi akaamua kuhamia kijiji kiitwacho Seke kwa Mtemi Mahizi ambako aliendelea kucheza ngoma na kufanya miujiza yake.

Akiwa Seke wilayani Kishapu ,mkoani Shinyanga; Mwanamalundi alifanya muujiza uliomuongezea heshima kijijini Seke. 

Wanakijiji cha Seke waliibiwa ng'ombe wengi sana na Wamasai kutoka Tabora. Wanakijiji wakataka kwenda kufuatilia ng'ombe hao usiku huo huo jambo ambalo Mwanamalundi alikataa. 

Mwanamalundi aliwahakikishia wanakijiji kuwa ng'ombe hao wapo salama na watarudishwa salama tu kesho asubuhi na sio usiku huo. Wanakijiji walikubali kutokana na kumuamini Mwanamalundi.

Usiku wa siku hiyo, Mwanamalundi akatuma nguvu zake zilizowazingira Wamasai na kisha kuwafanya wasinzie na mifugo hiyo. Hata walipofuatwa asubuhi, walikutwa wamelala fofofo. Wanakijiji wakawaua Wamasai hao na kisha wakarudi na mifugo yao.

 Mwanamalundi akapewa jina jingine ugenini na kuitwa "Kishosha mang'ombe ga Seke", ikimaanisha "Aliyerudisha ng'ombe za Seke".

Kuna kipindi, Mwanamalundi alivamia pori la Mtemi wa Ng'hung'hu aitwae Chalya ili achimbe mizizi fulani ya dawa.

 Mtemi Chalya alipata machale kuwa kuna mvamizi katika mapori yake anachimba mizizi ya dawa. Mtemi akaondoka na kuelekea kule ambako machale yalimuelekeza. Ni kweli, akamkuta Mwanamalundi akichimba mizizi ya dawa fulani.

 Mtemi akamuuliza Mwanamalundi, "ni kwanini umeingia katika utemi wangu bila kunijulisha?" Mwanamalundi akajibu, "Wewe ni mtemi wa watu wote ila mimi ndiye mtemi wa miti yote!" Jibu hilo lilimkwaza Mtemi Chalya ambaye aliamua kurudi kwenye himaya yake kwa ghadhabu na kuwaamuru askari wake wamkamate Mwanamalundi ili aadhibiwe.

Askari wakiwa wameambatana na Mtemi Chalya walipofika porini eneo alilokuwepo Mwanamalundi, hawakumkuta.

 Badala yake waliwakuta simba wengi wakiwa wamelala eneo hilo. Ilibidi watimue mbio kujiokoa wenyewe dhidi ya simba hao walioanza kuwafukuza. Walipofika kwenye himaya ya Mtemi wakiwa salama, walimkuta Mwanamalundi amemaliza kula chakula chao na anaondoka.

 Ilibidi mtemi amuache tu Mwanamalundi aondoke bila kumbughudhi kwa lolote.

Mwanamalundi alifariki mwaka 1936 kwa maradhi ya kawaida na kuzikwa Ididi Jihu huko kijiji cha Seke wilaya Kishapu mkoa wa Shinyanga akiwa ana umri wa miaka 44.

 Tukio la kifo chake liliitwa "hang'witulo gwa shigela" ikimaanisha "Vita ya kuwakimbia wamasai". Hii ni kwa sababu wakati Mwanamalundi anakata roho, kulitokea kishindo kikubwa kama tetemeko la ardhi. Watu wengi walikimbia ovyo kwa hofu kuwa labda wamasai wamevamia eneo lao ili kuwaua.

Baada ya kishindo hicho, giza likaingia ghafla, giza ambalo hata kuku wakaanza kurudi nyumbani, fisi wakaanza kutembea mitaani wakidhani ni usiku. Hata baada ya mazishi yake, kaburi lake lilifuka moshi mwingi sana uliopanda mpaka juu mawinguni na kutengeneza giza la muda mfupi.

 Mwanamalundi anakumbukwa pia kwa kuweza kutembea hewani bila kukanyaga ardhi, kujibadili na kuwa kiumbe tofauti kama mnyama, ndege, majani, mti au jiwe na uwezo wake wa kutembea juu ya maji au kuwa ndani ya maji kwa muda mrefu. 

Mwanamalundi ni mmoja tu wa watu mashuhuri katika tawala za Kisukuma. Kuna watu mashuhuri kabla yake kama akina Níndwa, Italange na Sïta. Hawa wote walikuwa ni watu wa miujiza kama alivyokuwa Mwanamalundi.

Makala hii inasimuliwa na Msukuma halisi na mwanahistoria ya Wasukuma Ngh'wana Ibengwe Shileki Mazege katika kitabu chake kiitwacho "Miujiza ya akina NG'WANA MALUNDI", toleo la kwanza 2015. Huyu Bwana ana vitabu vingi sana kuhusu historia ya wasukuma.

Kwa maswali yoyote kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana nae kupitia:

+255 763 379 387

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527