MWANAHARAKATI MAARUFU WA USHOGA AFARIKI DUNIA

Mwanaharakati wa kupigania haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya Binyavanga Wainaina amefariki dunia. Nduguye James Wainaina amethibitisha kwa BBC.

Mwanaharakati huyo amefariki akiwa na umri wa miaka 48.

Nduguye Binyavanga amsema kuwa familia yake inataka kusherehekea maisha yake , baada ya mwandishi huyo wa Kenya kufariki usiku wa Jumanne alipokuwa akiugua

''Tunasherehekea maisha yake, tunaangazia swala hili kibinaadamu .Turuhusu ule ubinaadamu kung'aa, kwa kuwa watu wanaomboleza'', Nduguye James alizungumza na mwadishi wa BBC Peter Mwangagi.

''Alifariki jana usiku katika hospitali moja alipokuwa akiugua. Lakini hicho ndicho kilicho kwa sasa tunajaribu kukubali habari hiyo'', aliongezea.

James amesema kuwa ijapokuwa habari za kifo cha nduguye tayari zimejaa katika mitandao ya kijamii , familia inajaribu kuwaelezea wale wasiojua.

James alisema kuwa Binyavanga hajakuwa katika afya nzuri katika kipindi cha miaka michache iliopita na hali yake ilikuwa imedorora katika kipindi cha kati ya miezi miwili au mitatu.

Nduguye hatahivyo alikataa kufichua ugonjwa uliosababisha kifo chake.

James anasema kwamba familia yake ilikuwa ikitumai kwamba Binyavanga atapona lakini hilo halikufanyika licha ya juhudu za madaktari.

Wainaina alikuwa mshindi wa tuzo ya Caine na aliorodheshwa na gazeti la Times magazine miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani 2014.

Amefariki siku mbili tu kabla ya mahakama nchini Kenya kutoa uamuzi wa iwapo itafutilia mbali sheria za kikoloni ambazo zinaharamisha haki za wapenzi wa jinsia moja.

Binyavanga Wainaina, alikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kujitokeza hadharani na kusema kuwa yeye hushiriki mapenzi ya jinsia moja.

Tangazo hilo lilimfanya Binyavanga kuwa mmoja wa waafrika mashuhuri kujitokeza hadharani.

Alifichua hali hii katika taarifa yake kupitia kwa mtandano wa kijamii wa Twitter iliowiana na siku ya kuzaliwa kwake.

Kifo chake kinajiri wakati ambapo kuna mjadala mkali nchini Kenya na katika baadhi ya mataifa ya Afrika kuhusiana na suala la haki za wapenzi wa jinsia moja.

Uamuzi wa Binyavanga kujitokeza hadharani ulipokelewa kwa hisia mbali mbali nchini Kenya. Kuna wale waliompongeza ingawa baadhi walihisi huenda jamii ikamtenga.

Mwaka 2018 Binyavanga Wainaina ambaye ni mwandishi maarufu wa vitabu aliwashangaza Wakenya wengi alipotangaza atafunga ndoa na raia wa Nigeria.

Alinukuliwa akisema: Nilimuomba mpenzi wangu tufunge ndoa wiki mbili zilizopita. Na alikubali, karibu mara moja. Yeye ni raia wa Nigeria. Tutakuwa tunaishi Afrika Kusini ambapo atakuwa anahudhuria masomo mwaka ujao. Tutaoana huko, mapema mwaka ujao," Bw Wainaina aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.


Aliahidi kwamba kutakuwa na karamu kubwa kwa Wakenya jijini Nairobi

Baadaye, aliongeza kwamba ana uhakika kutakuwa na sherehe kubwa kwa Wanigeria pia.

"Hakuna lililonishangaza zaidi kuliko kupendana na mtu huyu, ambaye ni mpole na mwenye moyo wa ukarimu'', alinukulkiwa akimsifu ,mpenzi wake.

"Najichukulia kuwa mwenye bahati sana kwamba yeye ananipenda na tulipendana majuzi tu, lakini tumefahamiana na tumekuwa tunachumbiana tangu 2012."

Binyavanga ni nani?
Kenneth Binyavanga Wainaina ambaye ana umri wa miaka 48 ni mwandishi wa vitabu na mwanahabari.

Mwaka 2002 alishinda tuzo mashuhuri ya uandishi kuhusu Afrika ya Caine.

Jarida la Time mwaka 2014 lilimuorodhesha Wainaina kuwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi zaidi duniani.
Mnamo 1 Desemba, 2016 alitangaza kupitia Twitter Siku ya Ukimwi duniani kwamba alikuwa ana virusi vya Ukimwi.
CHANZO - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527