Shuhudia Picha : MAELFU WAJITOKEZA KUUPOKEA MWILI WA MAREHEMU DR. MENGI DAR

Jeneza lenye Mwili wa marehemu Dk. Reginald Mengi ukiingizwa kwenye gari maalumu baada ya kuwasili nchini nchini ukitoa Dubai, tayari kwa safari ya kuelekea Hospitali ya Jeshi Lugalo, jijini Dar es salaam kwa kuhifadhiwa.

Na Said Mwishehe na Richard Bukos

MAELFU ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam leo Mei 6,2019 wamejitokeza kwa wingi kuupokea na kuulaki mwili wa aliyekuwa mfanyabishara maarufu nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Dk. Reginald Mengi ambaye amefariki dunia Mei 2 mwaka huu akiwa Dubai.

Mwili wa marehemu Dk.Mengi umewasili nchini saa nane mchana ambapo viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wastaafu na wananchi wa kada mbalimbali walijitokeza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kuupokea.

Pia Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete alikuwa miongoni mwa waliofika uwanjani hapo kuupokea mwili huo wa Dk.Mengi. Baada ya kuwasili na kupokelewa na kufanyika maombo kabla ya kuanza safari ya kuelekea Hospitali ya Lugalo.
Mjane wa Marehemu Dkt. Mengi, Bi. Jacquenine akiwana wa waombolezaji wengine pamoja na Mke wa Rais Mstaafu wa awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, Mama Salma Kikwete waliofika kwenye uwanja wa ndege wa J.K. Nyerere kumlaki.

Maelfu ya wananchi waliamua kuweka kambi katika barabara ambazo mwili wa Mengi umepitishwa ambapo wapo baadhi ya wananchi walionekana wakigusa jeneza ambalo limebeba mwili kama ishara ya kuonesha upendo.

Wakati mwili unapitishwa katika barabara ya Nyerere, Buguruni, Ilala,Kigogo, Magomeni, Kinondoni na Morroco wakati ukielekea Mwenge na kisha Lugalo idadi ya watu ilizidi kuongezeka kuusubiri mwili wa Dk.Mengi.

Simanzi na majonzi yalikuwa yametawala katika nyuso za wananchi walioamua kwenda kuulaki mwili wa Dk.Mengi huku wengi wao wakionekana kukimbilia gari iliyobeba mwili huo kwa lengo la kulishika. Mengi enzi za uhai alijipambanua kuwa karibu na jamii ya Watanzania ambapo alitumia sehemu ya fedha zake kutoa misaada.
Kutokana na idadi ya watu waliokuwa wamejipanga barabarani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliyekuwa kwenye msafara huo alionekana akihakikisha msafara huo unakwenda katika mazingira yaliyotulivu huku akisaidiwa na Jeshi la Polisi kupita Kikosi cha Usalama barabarani.

Katika msafara huo waendesha bodaboda nao hawakuwa nyuma kwani nao walikuwa sehemu ya wananchi ambao walihakikisha wanakuwepo katika mapokezi ya mwili huo.

Wananchi mbalimbali ambao walikuwa barabarani na kupata fursa ya kumzungumzia Dk.Mengi wamesema kuwa na mambo mengi ya kujifunza kutoka katika maisha ya Mengi ambaye enzi za uhai wake alikuwa na upendo kwa kila mtu na kubwa zaidi alihakikisha utajiri wake unawanufaisha na wengine kwani hakuwa mchoyo.

Maelfu ya wananchi walijipanga katika barabara za Jiji la Dar ambako mwili huo ulikuwa ukipitishwa na msafara kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi katika Hospitali ya Lugalo ambako utahifadhiwa kabla ya kuagwa kesho na kuzikwa Alhamisi.

Wananchi hao waliokuwa na nyuso za huzuni huku wengi wao wakimwaga machozi kwa kukumbuka mema aliyokuwa akiyafanya hapa nchini ikiwemo kuwasaidia vijana, wazee, watu wenye ulemavu na makundi mbalimbali yenye uhitaji, jambo ambalo limeonekana kugusa wengi.


Aidha, mbali na kuonyesha huzuni zao, wananchi hao walizingira msafara huo na kuzia gari ili waeze kuuona mwili wa mzee Mengi na baada ya hapo walianza kulisukuma gari hilo kama ishara ya upendo wao kwa Mzee Mengi aliyekuwa nembo kubwa kwa taifa hususani katika kuwakwamua vijana na watu wasiojiweza.
Sehemu ya waombolezaji wakiwa wamejitokeza kwa wiki maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam kuulaki mwili wa marehemu Dk. Reginald Mengi uliowasili nchini mchana wa leo. 
Mjane wa Marehemu Dkt. Mengi, Jacqueline Mengi akilia kwa uchungu.PICHA NA RICHARD BUKOS | GPL

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post