Picha : WAANDISHI WA HABARI,WADAU WA HABARI SHINYANGA WAADHIMISHA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI


Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga 'Shinyanga Press Club - SPC) imeadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani na kutaka usalama wao uzingatiwe kwenye kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika  mwezi Oktoba mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.

Maadhimisho hayo yamefanyika leo, Mei 3, 2019 kwenye ukumbi wa mikutano wa Liga Hoteli Mjini Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akimwakilisha mkuu wa mkoa huo Zainab Telack  na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa habari mkoani Shinyanga wakiwemo viongozi wa kidini, siasa, makampuni,serikali na taasisi zisizo za kiserikali.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mkuu huyo wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amewataka wanahabari mkoani Shinyanga kutumia kalamu zao vizuri kuhamasisha amani na utulivu vitawale kwenye kipindi cha uchaguzi wa Serikai za mitaa na uchaguzi mkuu ujao, ili wananchi waweze kuchagua viongozi wanaowataka kuwaletea maendeleo bila ya kubughuziwa.

“Kauli mbiu yenu ya maadhimisho ya uhuru wa habari mwaka huu 2019 'ya “Jukumu la UTPC na Klabu za Waandishi wa habari kuchangia uchaguzi huru na haki”,
 imekuja kwa muda muafaka, ikiwa tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa ambapo waandishi wa habari ni kiungo muhimu kwenye uchaguzi huu ikiwamo kutoa taarifa kwa wananchi pamoja na kudumisha amani,”amesema Mboneko.

“Hivyo nawaomba waandishi wa habari muitumie kalamu yenu vizuri sana kwenye kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kutoa taarifa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kupiga kura, pamoja na kulinda amani kwenye uchaguzi,”ameongeza Mboneko.

Pia amewataka waandishi wa habari kujikita kuandika habari kwa wingi zenye kuhamasisha wawekezaji wa viwanda kwenda kuwekeza mkoani Shinyanga ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Shinyanga.

Kwa upande wake Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Lutusyo Mwakyusa, amewatoa wasiwasi waandishi wa habari na kuhusu usalama wa waandishi wa habari wakati wa uchaguzi akibainisha kuwa usalama utakuwepo juu yao kwenye kipindi hicho cha uchaguzi wa Serikali za mitaa na kutoa wito kwao huku akiwakumbusha kuwa  kutokiuka miiko na maadili na taaluma zao.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga Shabani Alley, akisoma hotuba ya Klabu hiyo, amewaomba viongozi wa Serikali kufanya kazi kwa ukaribu na waandishi wa habari, ili kuutangaza mkoa huo pamoja na kudumisha amani na utulivu ili upate kukua kimaendeleo.

"Waandishi wa habari mkoani Shinyanga tumejipanga vyema kushirikiana na serikali, wanasiasa na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao unakuwa wa haki,tunaomba tuendelee kushirikiana ili kuhakikisha mkoa wetu unakuwa salama na kukua kimaendeleo",aliongeza Alley.

Maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu 2019 yana kauli mbiu isemayo “Jukumu la UTPC na Klabu za waandishi wa habari kuchagia uchaguzi huru na haki” ambapo wadau wa habari na waandishi wa habari mkoani Shinyanga pia wamejadili pia kuhusu usalama wa mwandishi wa habari katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu na umuhimu wa vyombo vya habari katika uchumi wa viwanda.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari mkoa wa Shinyanga yaliyoandaliwa na Shinyanga Press Club. Mboneko aliwataka waandishi wa habari mkoani humo kutumia kalamu zao kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kupiga kura ili kuchagua viongozi sahihi pamoja na kudumisha amani. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ,Shaban Alley,kulia ni Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Lutusyo Mwakyusa. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiwataka waandishi wa habari mkuano Shinyanga kujikita pia kuandika habari za kuchochea uwekezaji wa viwanda ili kukuza uchumi wa mkoa.


Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Shinyanga Shabani Alley akisoma hotuba ya Klabu hiyo siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani mwaka 2019.


Awali kabla ya kuanza kwa maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Shinyanga, mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiongoza Sala ya kumuombea Mmiliki na Mwanzilishi wa Makampuni ya IPP MEDIA Dkt. Reginald Mengi ambaye amefariki dunia jana akiwa Dubai kwa matibabu.Dkt. Mengi ni miongoni mwa watu ambao wana mchango mkubwa sana kwenye Tasnia ya Habari.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga Lutusyo Mwakyusa akiwahakikishia usalama wao waandishi wa habari kwenye kipindi cha uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao 2020.

Mkurugenzi msaidizi wa Radio Faraja FM Stereo Mjini Shinyanga Anikazi Kumbemba ambaye pia ni Mwandishi Mwandamizi akielezea dhumuni la maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Waandishi wa habari Mkoani Shinyanga wakiwa kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari.

Waandishi wa habari mkoani Shinyanga pamoja na wadau wakiwa kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari.

Wadau wa habari Mkoani Shinyanga wakiwa kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Shinyanga yakiendelea.

Waandishi wa habari na wadau wakiwa kwenye maadhimisho siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Shabani Katambi ambaye ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini akichangia mada kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani mkoani Shinyanga.

Afisa maendeleo ya jamii manispaa ya Shinyanga Octavina Kiwone akichangia mada kwenye maadhimisho siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani na kuwataka waandishi mkoani Sinyanga wakijikite pia kuandika habari za kuhamasisha utalii ili Serikali iweze kupata mapato.

Diwani wa Kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ntobi (CHADEMA)akichangia mada kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani mkoani Shinyanga na kuwataka waandishi wa habari mkoani humo, waandike pia habari ya kufufua kiwanda cha Nyama ambacho hakifanyi kazi katika manispaa hiyo.

Waandishi wa habari na wadau wa habari wakiendelea kusikiliza uchangiaji wa mada kwenye maadhimisho hayo ya uhuru wa vyombo vya habari.

Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel Maguja akichangia mada kwenye maadhimisho ya uhuru wa habari na kuwataka wanahabari wajikite pia kwenye maadili pale wanapokuwa wakiandika habari zao ili kuepuka kujiingiza kwenye matatizo.

Mdau wa habari Chief Abdala Sube naye akichangia mada kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari na kuvipongeza vyombo hivyo namna vinavyofanya kazi ya kutetea maslahi ya wananchi kwa kutatua kero zao.

Mwenyekiti wa mtaa wa Dome manispaa ya Shinyanga Solomoni Najulwa 'Cheupe', akivipongeza vyombo vya habari namna vilivyosaidia kuunyosha mtaa huo ambapo ulikuwa ukikabiliwa na changamoto nyingi.

Waandishi wa habari wakiwa na wadau wa habari kwenye maadhimisho ya uhuru wa habari wakisikiliza uchagiaji wa mada mbalimbali.

Mwandishi wa habari wa Gazeti la Uhuru Chibura Makorongo akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya uhuru wa vyombo vya habari, na kuwataka viongozi wa Serikali waboreshe mahusiano mazuri na wana habari ili kutangaza fursa za mkoa.

Wadau wa habari Mkoani Shinyanga wakiwa kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Waandishi wa habari mkoani Shinyanga wakipiga picha ya pamoja na wadau wa habari mara baada ya kumaliza kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527