MCHUNGAJI MSIGWA AHOJI UHALALI WA SPIKA NDUGAI KUMSIMAMISHA MASELE BUNGE LA AFRIKA


Makamu wa kwanza wa rais wa Bunge la Afrika,Mhe.Stephen Masele akiwa ofisini kwake katika makao makuu ya Bunge la Afrika,Johannesburg nchini Afrika Kusini
***
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amehoji nafasi ya wabunge wanaochaguliwa na Bunge kuwawakilisha katika mabunge mbalimbali duniani kusimamishwa na Spika bila uamuzi huo kujadiliwa na waliowachagua.

Akizungumza bungeni leo Ijumaa Mei 17, 2019 baada ya kuomba mwongozo kwa mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, mbunge huyo wa Iringa Mjini amesema uko wapi uhalali wa kiti cha spika kuwasimamishwa wawakilishi waliochaguliwa na chombo hicho cha kutunga sheria.

“Uhalali unatoka wapi na hawa hawakuteuliwa wamechaguliwa na nilitaka kujua anasimamishwa na kiti bila kujadili inatuchafua kama Taifa. Bunge litakuwa na nguvu gani ya kuwalinda hawa tunaowachagua,” amehoji Mchungaji Msigwa.

Ingawa Mchungaji Msigwa hakumtaja aliyekuwa akimlenga, lakini jana Alhamisi, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza kusimamisha uwakilishi wa mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele katika Bunge la PAP akimtuhumu kwa utovu wa nidhamu.

Ndugai alimtaka Masele ambaye ni makamu wa kwanza wa Rais wa PAP kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na kamati ya maadili ya CCM.

Akijibu mwongozo huo, Chenge amemtaka Mchungaji Msigwa kutowahisha hoja kwa maelezo kuwa tayari jana Alhamisi, Spika Job Ndugai alilitolea uamuzi kwa kuomba wabunge wasubiri taarifa itakapowasilishwa bungeni watakuwa na nafasi ya kujadili kwani milango haijafungwa.

Na Ibrahim Yamola - Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527