Mazungumzo kati ya Marekani na China yaambulia patupu

Mvutano wa kibiashara umeendelea kati ya Marekani na China huku nchi hizo zikitoa kauli zinazokinzana wakati ambapo Rais Trump ameamua kuongeza ushuru maradufu kwa bishaa za China.

China na Marekani zinatoa taarifa zinazotofautiana juu ya mazungumzo ya biashara. China imesema bado ina matumaini kuhusu kuutatua mvutano wa kibiashara, wakati Marekani imesema imeongeza ushuru mara mbili kwa bidhaa kutoka China. Hata hivyo mjumbe wa China katika mazungumzo na Marekani Liu He ameonya kwamba kuna viwango ambavyo nchi yake haitakuwa tayari kuvivuka.

Makamu wa waziri mkuu wa China Liu He amesema mazungumzo kati ya nchi yake na Marekani hayajavunjika licha ya kuwepo vikwazo vidogo ambavyo ni vya kawaida na kwamba China itaendela kuwa na mtazamo chanya juu ya mazungumzo ya biashara na Marekani, licha ya Rais Trump kuamua kuziongezea ushuru bidhaa za China.
 
Maoni ya Liu yanakinzana na ya waziri wa fedha wa Marekani Steve Mnuchin, ambaye aliwaambia waandishi wa habari wa CNBC kwamba hakuna mazungumzo yoyote ya biashara yaliyopangwa kufanyika kati ya nchi hizo mbili kwa sasa.

Rais wa Marekani Donald Trump amejisifu kwa kuandika kwenye Twitter kwamba ameikomoa China kwa kiasi ambacho labda nchi hiyo haitotaka kurudi kwenye meza ya majadiliano kabla ya uchaguzi wa 2020.

Marekani imechochea vita vya biashara kwa kuongezaushuru kwa thamani ya dola bilioni 200 kwa bidhaa za China zinazoingia nchini humo. Wachambuzi wa China wamesema huenda Marekani haina utayarifu kwa kile inachoweza kuhimili.Gazeti la kizalendo la Global Times limeandika kwenye tahariri yake kwamba Marekani haijatambua maslahi ya pande zote mbili, na wala haizingatii kwa kiasi kikubwa uvumilivu wa China.

Mnamo siku ya Ijumaa, Rais Donald Trump aliweka vikwazo vipya dhidi ya bidhaa zinazoingia Marekani kutoka China. 

Hatua hiyo iliongeza ushuru kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 kwenye bidhaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na simu za mkononi, kompyuta na vitu vya kuchezea watoto. Wizara ya Biashara ya China imesema imehuzunishwa mno na uamuzi wa Marekani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post