LUKUVI APUKUTISHA MAOFISA ARDHI MKOA MZIMA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi William Lukuvi, ameagiza kuhamishwa watumishi wote wa Sekta ya ardhi katika mkoa mzima wa Morogoro sambamba na kuanzishwa ofisi ya Ardhi Kanda ya Mashariki katika mkoa huo.

Lukuvi amesema baada ya kutembelea Wilaya ya Kilosa amebaini watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo wamejisahau na njia pekee ya kufanya ni kuwaondoa  watumishi wote wa sekta hiyo na kuwapeleka maeneo mengine kwa lengo la kupata watendaji wapya.

"Majaribio mengi yamefanyika katika mkoa wa Morogoro kama vile kupanga na kupima kila kipande cha ardhi, utoaji hati za kimila pamoja na uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli  kufuta mashamba makubwa yasiyoendelezwa, lakini mambo katika sekta ya ardhi kwenye mkoa huo hayaendi"  alisema Lukuvi.

Aidha, Waziri Lukuvi alisema, kutokana na mkoa wa Morogoro kuendelea kuwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu ameamua kuirejesha kanda ya Mashariki ambayo sasa itakuwa kanda maalum ya ardhi kwa mkoa huo, itakayokuwa na  wataalamu wote wa sekta ya ardhi  akiwemo Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda,  Wapima, Wathamini pamoja na Wataalamu wa Mipango Miji.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, kuanzishwa kwa kanda maalum Morogoro kutaufanya mkoa huo kuwa mkoa pekee Tanzania wenye kanda ya ardhi na kubainisha kuwa ofisi hiyo itatakiwa kuanza kazi mapema mwezi Julai 2019.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero Yusufu Athuman, alisema wilaya hiyo inazo changamoto kubwa katika masuala ya ardhi kwa kuwa wananchi wa wilaya hiyo wana uhitaji mkubwa wa ardhi na sehemu kubwa ya ardhi katika wilaya hiyo iko kwa watu wachache.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post