LUGOLA ATANGAZA KIAMA KWA TRAFIKI WANAO WABAMBIKIZIA MAKOSA MADEREVA


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewatangazia kiama askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini wanaowabambikia madereva makosa ya picha za mwendokasi (Speed rader) zisizo na uhalisia kwa nia ya kujipatia mapato wakibainika watawajibika kuzilipa wao wenyewe faini hizo na kuondolewa katika kitengo hicho.


Alitoa agizo hilo mjini Morogoro wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maafikiano kati ya vyama vya watoa huduma za usafirishaji nchini kuhusu kusitisha kusudio la madereva wa mabasi ya abiria kufanya mgomo wakishinikiza kutimiziwa madai yao mbalimbali ikiwamo ya mikataba ya kazi.

Alisema maamuzi hayo yametokana na makubaliano ya pamoja baina viongozi wa vyama hivyo vya usafirishaji pamoja na wizara mtambuka za serikali kwa nia ya kutatua changamoto walizowasilisha katika kikao hicho kuhusu kubambikiwa makosa na askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani.

Waziri Lugola, alisema moja ya makosa yanayolalamikiwa na madereva hao ni pamoja tochi zinazopiga picha mabasi na kurushwa kwenye simu za maaskari zinakosa uhalisia wa tukio ikiwamo kutoonekana kwa namba za usajili pamoja na vibao vya kuzuia makatazo mbalimbali na kusababisha utata na mivutano yenye nia ya kujenga mazingira ya rushwa.

Alisema kuanzia sasa askari hao wanapaswa kupiga picha katazo mbalimbali za barabara mbele ya gari ikionyesha mwonekano usio na mashaka, namba ya usajili pamoja na eneo la alama iliyokiukwa na dereva ili kuwapo na ushahidi halali vinginevyo dereva huyo asichukuliwe hatua yoyote.

“Dereva anapokuwa na mashaka na picha iliyopigwa dhidi ya gari lake kama haionyeshi usajili wa namba za gari na eneo la kibao cha zuio asikubali kuadhibiwa na badala yake amweleze huyo askari azitume picha hizo kwa msimamizi wa kikosi cha usalama barabarani na aende huko,” alifafanua Waziri Lugola.

Pia alisema tabia ya baadhi ya askari kukamata mabasi yenye abiria na kuyafikisha kituo cha polisi kwa nia ya kumuadhibu dereva aliyetenda makosa, jambo hilo liachwe mara moja na badala yake dereva aliyetenda kosa anapaswa kukamatwa katika kituo cha mwisho cha safari yake.

“Sheria ya Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), inaeleza wazi kila basi linalofanya safari za masafa marefu lazima liwe na madereva wawili, hivyo ukimkamata dereva na kumweka ndani tayari unaenda kinyume na sheria za Sumatra na kulifanya basi kushindwa kuendelea na safari yake,” alisema.

Aidha, aliliagiza Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea kuwanyang’anya leseni madereva wanaofanya makosa ya kujirudia pamoja na kukamata magari yanayofanya shughuli za usafirishaji bila kuwa na leseni kwa kushirikiana na Sumatra.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post