LIPULI FC YAICHARAZA YANGA 2 - 0


Timu ya Lipuli FC ya Iringa imefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya vigogo, Yanga SC Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Sasa Lipuli FC itamenyana na Azam FC katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo itakayofanyika Uwanja wa Ilulu mjini Lindi mapema mwezi ujao. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Shomary Lawi wa Kigoma, mabao ya Lipuli FC yalifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Paul Nonga dakika ya 27 na Daruwesh Saliboko dakika ya 38.

Wazi Yanga haitashiriki michuano ya Afrika mwakani baada ya kipigo cha leo, kwani kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara ubingwa umekaa vizuri zaidi kwa watani waol Simba SC.

Na kipigo hiki kinakuja siku moja baada ya kuchaguliwa kwa uongozi mpya wa klabu chini ya Mwenyekiti, Dk. Mshindo Mbette Msolla, Makamu Mwenyekiti Frederick Mwakalebela na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Hamad Islam 1,206, Mhandisi Bahati Faison Mwaseba 1,174, Dominick Ikute, Kamugisha Kalokola, Arafat Haji, Salum Ruvila, Saad Khimji na Rodgers Gumbo.
Uchaguzi huu umefuatia kujiuzulu kwa viongozi wote waliongia madarakani Juni 11 mwaka 2016, Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wao, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay, Hussein Nyika, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Inspekta Hashim Abdallah.

Kikosi cha Lipuli FC kilikuwa; Yusuph Mohammed, Haruna Shamte, Paul Ngalema, William Lucian ‘Gallas’, Ally Sonso, Freddy Tangalu, Miraj Athumani ‘Madenge’/Novaty Lufunga dk81. Jimmy Shoji, Paul Nonga, Dariwesh Saliboko na Zawadi Mauya/Steven Maganga dk89.

Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Mwinyi Hajji Mngwali, Abdalla Shaibu ‘Ninja’, Andrew Vincent ‘Dante’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Mohammed Issa ‘Banka’/Amissi Tambwe dk47, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na Ibrahim Ajibu/Juma Abdul dk60.
Chanzo -Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527