KATIBU MKUU CCM DK. BASHIRU AMUOMBEA RADHI MAKONDA KWA KAULI ZAKE.....ASKOFU SHOO AMPATANISHA NA MBOWE


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally amemuombea msamaha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutokana na kauli yake aliyoitoa wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni tanzu za IPP, Dk. Reginald Mengi katika viwanja vya Karimjee.

Katika kauli yake iliyozua sintofahamu, Makonda alisema hajawahi kuona mtu yeyote wa kabila la wachaga akitoa msaada au fedha kwa walemavu.

Kauli ambayo haikuwapendeza watu wengi akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ambaye wakati akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kuaga mwili wa Dk. Mengi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro leo Alhamisi Mei 9, alikumbushia suala hilo na kuwataka Watanzania kutogawanywa kwa kauli na vitendo vya kibaguzi zinazotolewa na viongozi.

Akizungumza wakati akitoa salamu za rambirambi, Dk. Bashiru amesema kauli za Makonda zimesababishwa na wao kama walezi kushindwa kutoa malezi ya kutengeneza viongozi bora.

Dk. Bashiru amesema hayo baada ya kauli ya Askofu Mkuu wa KKKT Usharika wa Kaskazini, Fredrick Shoo kuzungumzia umuhimu wa kuwaandaa viongozi bora, watiifu na wanyeyekevu.

“Naomba nitumie fursa hii kumuombea msamaha kijana wangu Makonda, mimi namfahamu na hii ni mara yangu ya pili nimemsema hadharani, mara ya kwanza nilimsema Simiyu akaja analia ofisini nikamwambia ubadilike na kwa kweli ameanza kubadilika.

“Bado ni kijana mzuri shupavu na bado tunahitaji, lakini tunahitaji kuwasaidia vijana wetu,” amesema Dk. Bashiru.

Hata hivyo baada ya Dk. Bashiru kumaliza kuzungumza, Askofu Shoo alimuita Makonda na kumuombea msamaha kisha akawapatanisha na Mbowe.

“Makonda uko wapi? njoo tunakutangazia msamaha hapa hapa na nimekusamehe na hapa ni madhabahuni nimewaita kw ajili ya upatanisho,” alisema Askofu Shoo.

Aidha baada ya kuombewa msamaha Makonda aliwashukuru Dk. Bashiru na Askofu Shoo kwa kumuombea msamaha.

“Kwanza nashukuru kwa maelekezo na maonyo ya baba Askofu, na nashukuru kwa Katibu wangu Mkuu kwa kusimama na kuomba msamaha kwa niaba yangu lakini pia namshukuru kaka yangu Mbowe mimi na yeye tunafahamiana kwa muda mrefu na mbele ya baba yetu Mengi kwa kutamka yale yaliyomkwaza naye pengine angeweza kukaa kimya.

“Nahisi tafsiri inaweza kuwa tatizo naomba radhi kwa kumsifia mchaga katikati ya wachaga na si mchaga kati ya wengine na nitaendelea kumshukuru kwa yote aliyoyafanya katika mkoa wetu hususani kusaidia walemavu,” amesema Makonda.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post