MKUU WA WILAYA AWAPIGA STOP MANGARIBA NA WAGANGA WA JADI WASIO NA VITAMBULISHO VYA WAJASIRIAMALI


Na Bakari Chijumba, Lindi.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi, Hashim Mgandilwa amepiga marufuku wamiliki wa viwanja vya kucheza unyago kutumia Mangariba wasio na vitambulisho vya wajasiriamali wadogo.

Amesema hayo 23 Mei 2019, wakati wa kikao cha mangariba(Wanaotahiri watoto), waganga wajadi na wamiliki wa viwanja vya kuchezea unyago kilichofanyika ukumbi wa CCM Ruangwa mjini.

Mgandilwa amemtaka kila waganga wa jadi kuwa na kitambulisho cha mjasiriamali mdogo kama anataka kuendelea kutoa tiba katika Wilaya ya Ruangwa.

Mkuu huyo wa wilaya amesema wamiliki wa viwanja vya unyago wanapaswa kuzingatia ratiba ya kufunga na kufungua shule ili mtoto anafanyiwa unyago asikose haki ya kupata elimu.

"Msitafute shida,Halmashauri ikianza kutoa vibali vya sherehe hizo nitafuatilia kama umepokea watoto siku husika ya tarehe 8 mwezi wa 6 na kumaliza tarehe 6 mwezi wa  7 ikifika tarehe ya mwisho  watoto wote wawe wametoka Jando" amesema Mgandilwa.

Aidha Mgandilwa amewataka wazazi na wahusika wa shughuli za unyago, kuhakikisha watoto wanapokuwa jandoni wanalazwa kwenye vyandarua ili kuepusha maradhi na pia amesisitiza umuhimu kuzingatia usafi wa  maeneo ya viwanja vya unyago.

"Mnapofanya shughuli hizi zingatieni msingi ya afya kila mwenye kiwanja awe na uhakika na daktari ni vyema tukaangalia usalama wa watoto wetu" amesema  Mgandilwa

Mgandilwa amewataka pia wanaohusika  na shughulia za jando, kuzingatia  mafunzo  wanayotoa kwenye jando na unyago  yaendane na maadili ya kitanzania na umri wa watoto wanaopewa hayo mafunzo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post