AGIZO LA RAIS MAGUFULI NJOMBE LATEKELEZWA,STENDI KUU MPYA YAANZA KAZI

Na Amiri kilagalila-Njombe

Mkoa wa Njombe umeanza rasmi kutumia kituo kipya cha mabasi mjini Njombe ikiwa ni baada ya agizo la rais  John Pombe Magufuli alilotoa Aprili 10 akiwa mkoani humo kuwa kituo hicho kianze kazi baada ya siku 30.

Ujenzi wa kituo hiki unaofadhiliwa na benki ya dunia ulioanza 2013 umekuwa ukisuasua kwa kipindi kirefu licha ya uwepo wa fedha jambo ambalo lilimkasirisha Rais Magufuli na kuamua kutoa siku therathini kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe kukamilisha ujenzi huo.

Emmanuel George ambaye ni katibu tawala wilaya ya Njombe Yenye Halmashauri tatu ikiwemo mji Njombe,akizungumza mara baada ya kuanza Kutumika Kwa  kituo hicho mapema alfajiri amesema serikali imefanya jitihada za lazima kukamilisha mradi huo ambao umeanza kutumika licha ya kuwepo kwa baadhi ya maeneo machache ambayo hayaja kamilika huku akitaja faida zake kiuchumi.

"Licha kuanza kwake kuna changamoto ndogo ndogo ambazo tunaendelea nazo na leo ndio imeanza kufanya kazi, ni stendi kubwa na ya kisasa na itakuwa ni chachu ya kwenye mapato ya halmashauri,vitu ambavyo havijakamilika ni vichache kwasababu ya mvua"alisema katibu tawala

Baadhi ya madereva na abiria Akiwemo Michael Msilu na Amosy Kusalula wakizungumzia kituo hicho wamepongeza hatua zilizochukuliwa na serikali huku wakidai bado kuna changamoto ya miundombinu muhimu ikiwemo jengo la abiria na eneo la mama Lishe ambayo bado yanaendelea kujengwa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Iluminatha Mwenda Amesema Ujenzi wa Kituo Hicho Kipya Umefikia Asilimia 95 na Kwamba Zoezi la Ukamilishaji Linaendelea.

"Sasa hivi stendi yetu imekwishakamilika kwa asilimia 95 kama mnavyoona magari yamekwishaanza kuingia na hizi asilimia tano ndani ya wiki mbili tutakuwa tumekwisha kamilisha,na kama unavyo jua Njombe ni mvua sana tunaendelea kuomba ile sala ambayo tunasali kila siku ya toba basi iendelee kutusaidia ili mvua isiendelee kunyesha"alisema Iluminatha Mwenda

Ujenzi wa kituo hicho Kipya Cha Mabasi Mjini Njombe umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 9 za kitanzania Ikiwa Kila Mtu Anayeingia Ndani ya Kituo Hicho Anapaswa Kulipa Ushuru wa Shilingi 200 na Baada ya Mabasi Kutoka Ndani ya Stendi Hiyo Kituo Cha Kwanza Kwa Barabara ya Kwenda Makambako Kitakuwa Kibena Huku Wanaokwenda Songea Kikiwa Nundu .


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527