WAZIRI MKUU: SERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA CPA


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali itatoa ushirikiano kwa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika (CPA – Africa)wanaotarajia kufanya mkutano wao Novemba 2019, nchini Tanzania.

Ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Aprili 4, 2019) alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Chama cha Mabunge ya Madola Kanda ya Afrika, Mheshimiwa Emilia Monjolwa Lifaka.

Waziri Mkuu alisema Bunge na Serikali nchini wanafanya kazi kwa kushirikiana, hivyo amemuhakikishia Mhe. Emilia ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Cameroon kuwa Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika kwa CPA ili kufanikisha malengo tarajiwa

Pia, Waziri Mkuu alisema Serikali inaushukuru uongozi wa CPA kwa kutoa ushirikiano stahiki kwa wabunge wa Bunge la Tanzania ambao ni wanachama wa CPA

Kwa upande wake, Mhe. Emilia aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na kutoa fursa kwa wanawake katika nafasi za uongozi ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya wabunge wanawake kufikia asilimia zaidi ya 30 ya wabunge wote.

Kadhalika, Mwenyekiti huyo alisema Maspika wa CPA – Afrikawanaotarajia kufanya mkutano Novemba 2019, katika jiji la Arusha nchini Tanzania wameridhika sana kwa ahadi ya Serikali ya Tanzania kuhusu ushirikiano na maandalizi mazuri.

Mkutano huo wa Maspika wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika utajadili ajenda mbalimbali pamoja na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post