WAZIRI MKUU AKUTANA NA MWAKILISHI WA UNICEF TANZANIA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempongeza mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) kwa kazi kubwa iliyofanywa na Shirika hilo hapa nchini.

Ametoa pongezi hizo leo (Alhamisi, Aprili 11, 2019) alipokutana na mwakilishi wa UNICEF, Bibi Maniza Zaman ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amempongeza Bibi Zaman kwa upendo mkubwa aliouonesha kwa watoto wa Tanzania hasa katika kusimamia masuala ya afya, elimu na haki za watoto wa kike. “Tumenufaika na mengi kutoka UNICEF wakati ukiwa hapa hasa kwenye masuala ya haki za watoto,” amesema na kuongeza:

“Utendaji wako wa kazi katika nyanja hizi uliwezesha tufanye kazi kwa utulivu kwa sababu ulikuwa ukisukuma mambo mengi, kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. Tunasikitika kwamba utaondoka hivi karibuni lakini tunakutakia heri na maisha mema huko uendako Kenya.”

Kwa upande wake, Bibi Zaman ambaye amekaa hapa nchini kwa miaka mitatu na miezi minne, amesema anaishukuru Serikali kwa ushirikiano iliompatia kwa kipindi chote alichokuwa hapa nchini. “Ninaona siku zimeisha haraka sana, lakini ninashukuru viongozi mbalimbali kwa ushirikiano walionipatia,” amesema.

Amesema katika kipindi chote hicho, ameshirikiana vizuri na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, na wizara nyingine tano za kisekta ambazo amekuwa akifanya nazo kazi kwenye masuala ya watoto.

Bibi Zaman amesema jambo kubwa la kujivunia ni mafanikio yaliyopatikana kwenye kazi ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri usiozidi miaka mitano ambayo ilifanyika kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

“Tuliweza kuunda mfumo rahisi wa kusajili watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao iliwasaidia kupata vyeti ndani ya siku moja na tumeweza kuifikia mikoa 13 ambayo ni nusu ya mikoa yote hapa nchini. Kazi hii imewezesha watoto milioni 3.5 wapate vyeti vya kuzaliwa na kuongeza kiwango cha watoto wenye vyeti hivyo, iongezeke kutoka asilimia 13 hadi kufikia asilimia 38 katika kipindi cha miaka minne na nusu,” amesema.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Mwanza, Lindi na Geita. Mingine ni Shinyanga, Mara, Simiyu, Mtwara, Dodoma na Singida. Amesema ana imani kuwa kwa mikoa iliyobakia, kazi hiyo itakamilika pindi fedha zitakapopatikana.

Pia amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kupunguza tatizo la utapiamlo. Maeneo mengine ambayo wamefanyia kazi ni elimu na afya.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527