WAZIRI MKUU AKAGUA OFISI ZA SERIKALI MTUMBA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ofisi mpya za wizara saba katika mji wa Serikali ulioko Mtumba, Dodoma na kusisitiza waweke vibao vya ofisi na kukamilisha mazingira ya nje.


“Kuna wizara hazina majina kwa nje. Hakikisheni majengo yote yanawekwa majina haraka ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaokuja huku kutafuta huduma. Kama kuna wizara mbili ziko jirani, pale njia panda wekeni kibao kuonesha majina ya wizara zote mbili. Nia ya Serikaili ni kutoa huduma zote kutokea hapa Mtumba,” amesema.

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumanne, Aprili 23, 2019) wakati akitoa majumuisho ya ziara hiyo fupi kwa maafisa wa Serikali waliokuwepo kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara ya nishati ambako ndiko alimalizia ziara yake.

Waziri Mkuu ametembelea wizara saba ambazo ni Maliasili na Utalii; Ofisi ya Rais - TAMISEMI; OWM - Sera, Uratibu na Bunge; Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora; Mifugo na Uvuvi, Ulinzi na JKT na ya mwisho ilikuwani ni Wizara ya Nishati.

“Nimefurahi kukuta Mawaziri, Naibu wao na Makatibu Wakuu pamoja na wakuu wa idara wako huku na kazi zinaendelea, lakini ni lazima nisisitize kwamba idara zinazohamia huku ziwe ni zile zenye kutoa huduma za kila siku kwa wananchi,” amesema.

“Ni lazima tuwaeleze wananchi na wadau wetu ili watambue kwamba Serikali imehamia huku, lakini wakija kutaka huduma wasikute idara inayowahusu iko mjini au wengine wako huku na wengune wako kule.”

Kuhusu miundombinu ya barabara, umeme na TEHAMA, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma inasimamia kazi hiyo ikiwemo suala la ujenzi wa kituo kikubwa cha afya ambacho kitakuwa na huduma zote kwa viongozi lakini pia pia kitatoa huduma kwa wananchi waishio vijiji vya jirani.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka mawaziri walioko Mtumba wajiandae kwani kuna siku atakwenda kufanya vikao vyake kwenye wizara zao kwa sababu amebaini kuwa kila wizara ina ukumbi mkubwa wa mikutano.

Mapema, akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema jumla ya watumishi 64 wameshamia kwenye ofisi za wizara hiyo ambapo kuna vyumba 25 vya ofisi na ukumbi mmoja wa mikutano.

Pia alisema waligawa miche ya miti 13,570 kwa wizara mbalimbali na kwamba katika ofisi yake, wamepanda miti 980.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. Suleiman Jafo alisema wamekwishahamia tangu Jumatatu iliyopita na kwa sasa wanatumia ofisi za muda ambazo ni za mabati huku wakisimamia ujenzi wa ghorofa yao hadi ukamilike.

Akielezea kuhusu ujenzi wa ofisi hizo ulipofikia, Bw. Jafo alisema ifikapo mwishoni mwa wiki watakuwa wamekamilisha kazi ya kuweka mabati na kupiga plaster. “Tunatarajia kukamilisha kazi ya ujenzi Mei 30, kama ilivyopangwa. Jengo lilikamilika litakuwa na kumbi mbili za mikutano na ofisi za kuchukua watumishi 88,” alisema.

Naye Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema kuwa hadi sasa watumishi 73 kati ya 153 ndiyo wamehamia kwenye ofisi mpya za Mtumba.

Alisema kwa sasa wanatenegeza eneo la maegesho ya magari na wameshatenga eneo la mgahawa kwa ajili ya wafanyakazi wa wizara hiyo.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post