WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUCHAPISHA HABARI MTANDAONI BILA KUWA NA LESENI YA TCRA


Wafanyabiashara wawili ambao ni wakazi wa Kigamboni wamepandishwa mahakamani hapo kujibu shtaka la kuchapisha habari katika mtandao bila kuwa na leseni.

Washitakiwa hao ni Obadia Kwitega na Stella Ommary ambao wamesomewa shtaka lao  na  Wakili wa Serikali, Constantine Kakula mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwezile.

Wakili Kakula alidai kuwa washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 29 na Machi 29, 2019 katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam ambapo kupitia runinga ya mtandaoni ikijulikana kama Habari Mpya TV walichapisha taarifa bila kibali cha Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Washtakiwa baada ya kusomewa mashitaka hayo, walikana kutenda kosa hilo.

Wakili Kakula alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Rwezile alitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao ambapo kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya maneno ya Sh5milioni. Pia kila mshtakiwa anatakiwa kusaini dhamana ya maneno ya  Sh5milioni.

Hata hivyo, mshitakiwa Stella ndiye aliyeweza kutimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana, huku mwenzie akirudishwa rumande.

Hakimu Hamza aliahirisha kesi hiyo hadi  Aprili 30, 2019, itakapotajwa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527