TAIFA STARS YAPANGWA KUNDI C PAMOJA NA SENEGAL, ALGERIA NA KENYA AFCON 2019Hatua ya upangaji wa makundi ya michuano ya Afcon ya Afrika imepangwa leo nchini Misri ambapo tayari Tanzania imewajua wapinzani wake watakaomenyana nao mwezi Juni nchini Misri.

Hafla hiyo ambayo imehudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Wallace Karia pamoja na Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania, Emmanuel Ammunike yalishuhudiwa na Dunia nzima kupitia SuperSport

Pia ilihudhuriwa na nyota wa zamani kwenye soka kama Mustapha Hadji mchezaji wa zamani wa AS Villa na timu ya Taifa ya Morrocco, Eliaj Diof mchezaji wa zamani wa Liverpool na timu ya Taifa ya Senegal, nahodha nstaafu wa timu ya Misri Ahmed Hassan, nahodha mstaafu wa timu ya Ivory Coast na timu ya Barcelona Yaya Toure.

Tanzania imepangwa Kundi C Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) pamoja na Kenya, Algeria na Senegal.

Magwiji Mustapha Hadji wa Morocco, Ahmed Hassan wa Misri, El Hadji Diouf wa Senegal na Yaya Toure wa Ivory Coast waliongoza droo hiyo usiku huu kwenye ukumbi wa Sphinx & the Pyramids mjini Giza, Misri.

Wenyeji, Misri wapo Kundi A pamoja na Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wakati Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria.

Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F ni Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon.

Taifa Stars ilifuzu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano. 

Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.

Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo. 

Michuano itaanza Juni 21 hadi Julai 19 na Taifa Stars itachezea mechi zake Uwanja wa Juni 30 na Al Salam mjini Cairo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post