SHILINGI MILIONI 5 YA RAMBI RAMBI ILIYOTOLEWA NA RAIS MAGUFULI MKOANI NJOMBE YAKABIDHIWA


Na Amiri kilagalila-Njombe
Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka amekabidhi fedha ya rambi rambi kiasi cha shilingi milioni tano zilizotolewa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John pombe Magufuli  kwa familia tano zilizokumbwa na mauaji ya watoto yaliyotokea kuanzia mwezi wa kumi na moja mwaka jana.

Olesendeka amesema Rais Magufuli kwa niaba serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania amekabidhi fedha hiyo ya pole kwa familia zilizoondokewa na watoto kutokana na ahadi yake aliyoitoa wakati wa ziara yake ya siku tatu mkoani humo.

“Mheshimiwa Rais alipokuwa mkoani hapa kwa siku tatu hakuonyesha kuficha hasira zake na alionyesha kufedheheshwa na kukasilishwa kwa vitendo  vilivyokuwa vimefanyika kati ya mwezi wa kumi na moja na mwezi wa pili mwaka huu ambapo tulipoteza watoto wetu takribani watoto nane,lakini Rais amenielekeza nifike kwenye familia hizi na kuwashika mkono wa pole kwa niaba yake kwa kuongozana na kamati ya ulinzi na usalama”alisema Olesendeka

Aidha Olesendeka amewasisitiza viongozi wote wa wilaya ya Njombe na mkoa kwa ujumla kuhakikisha vitendo vya aina hiyo havirudiwi kwa mara nyingine.

“Nichukue nafasi kuwataka viongozi wa wilaya hii ya Njombe na katika mkoa wetu kwa ujumla wake hakuna mtu au mtoto yeyote atakayepoteza maisha yake kwa vitendo kama hivyo au kwa visingizio vyovyote vile”aliongeza Olesendeka 

Miongoni mwa familia zilizotembelewa ni pamoja na familia ya Bw.Daloti Nahala walioondokewa na mtoto Oliver Nahala,wameishukuru serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na wananchi kwa ujumla kuyaona matatizo hayo na kuyachukulia uzito.

“Mimi niwashukuru wa Tanzania na serikali nzima ya Tanzania kwa kuliona hili na kulichukulia uzito ili liweze kutulia na nchi yetu ibaki kuwa na amani” alisema Nahala mmoja wa wazazi waliondokewa na watoto

Familia tano zilizokumbwa na matatizo hayo zimekabidhiwa kiasi cha shilingi milioni moja kila familia kama pole iliyotolewa na Rais Mgufuli mkoani Njombe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post